Karagwe. Mzee mmoja mkazi wa Omurushaka Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Haruna Gabery (75) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na nyuki akiwa msikitini akifanya maandalizi ya swala ya jioni.
Gabery anadaiwa kufariki dunia akiwa msikiti wakati akijaribu kujiokoa baada ya kuvamiwa na nyuki waliyokuwa wametapakaa mtaa mzima kumzidi uwezo hadi kuingia puani na mdomoni, hatimaye kupoteza maisha.
Mkazi wa Mtaa Omurushaka, Abdul Molandi, muumini wa msikiti wa Istiqama Bakwata wilayani Karagwe, amesema tukio hilo lilitokea Jumatano Desema 11, 2024 katika Mtaa wa Omurushaka baada ya nyuki kutapakaa mtaa mzima na kuzua taharuki.
Molandi amesema nyuki hao siku za nyuma huo walikuwa wameweka makazi ndani ya nyumba moja ambayo hawaishi watu, lakini Jumatano iliyopita walitoka na kutapakaa mtaa mzima hadi msikitini.
Amesema alishuhudia mzee huyo akiingia msikitini kupitia mlango wa nyuma na kuchukua dawa ya wadudu kwa ajili ya kuwaua nyuki hao waliokuwa maeneo hayo ila hakufanikiwa na alipozidiwa na nyuki hao aliingia msikitini, watu walipofika walikuta amefariki dunia.
Awali, Sheikh wa Wilaya ya Karagwe, Alhaj Nasibu Abdu, alisema aliyefariki dunia ndani ya msikiti ni mzee wa msikiti huo wa Istiqama, Bakwata, Mtaa wa Omurushaka ambaye pia ni mtunza msikiti.
“Yeye alikwenda pale msikitini majira ya saa 10 na nyuki walikuwa wachache, lakini kutokana na umri wa mzee bila shaka aliporudi kuandaa swala ya alasiri, nadhani nyuki wawili, watatu walimshambulia na kupata mshtuko na mauti yakamkuta hapahapa msikitini,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Omurushaka, Ndibalema Kanyambo amesema Jumatano alipokea taarifa za tukio hilo na kufika msikitini ambako alikuta mtu huyo ameaga dunia.
“Nilikuta kweli amefariki dunia, nyuki walikuja ghafla na kuzingira mtaa wangu, lakini moyo wangu ulitaharuki sana maana nimempoteza shemeji yangu,” amesema.
Kanyambo amesema kwa sababu tukio hilo limetokea mtaani kwake, wanakwenda kufanya utambuzi wa nyumba zote ambazo haziishi watu ili kuweka usalama zaidi wa raia na mali zao.
Kanyambo ameongeza kuwa baada ya kukubaliana wao kama familia ya marehemu, mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda Kijiji cha Rongwe Kata ya Kasharu wilayani Muleba kwa maziko.