Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Hali ya Hewa na Maendeleo (CCDR) kwa Tanzania iliyozinduliwa na Benki ya Dunia (WB) imetaja hatua tano zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hizo ni kuwajengea watu uelewa wa kukabiliana na hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha matumizi sahihi ya maji katika kilimo na kuwekeza kwenye miundombinu rafiki kwa mazingira isiyozalisha hewa ukaa.
Mengine ni kuziongezea uwezo taasisi kushughulikia masuala ya tabianchi na kutumia mbinu bora za kupata ufadhili wa kifedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti hiyo imefafanua hatua hizo zinajumuisha kuimarisha ulinzi wa kijamii, kupanua upatikanaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na afya; kujenga mifumo ya elimu inayozingatia masuala ya tabianchi na kuunda nafasi za ajira rafiki kwa mazingira.
Pia, imesisitiza umuhimu wa kusaidia jamii zilizo hatarini kuwa na uwezo wa kuhimili mishtuko ya tabianchi.
Ripoti imeeleza kuboresha usimamizi wa ardhi na maji, kuwekeza katika teknolojia za kilimo zinazozingatia tabianchi na kuimarisha miundombinu imara ni hatua za msingi.
Hayo yanaelezwa yanapaswa kuambatana na kuongeza maarifa kuhusu mbinu bora za kilimo na kupata fedha za kuongeza uzalishaji, huku zikihifadhi mazingira.
Kwa mujibu wa ripoti, kushindwa kuchukua hatua hizo kunaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2050, kusababisha watu milioni 2.6 kuingia kwenye umasikini na kulazimisha wengine milioni 13 kuhama makazi yao ndani ya nchi.
Ripoti pia imesisitiza umuhimu wa kuunganisha masuala ya tabianchi katika mipango ya maendeleo ya Tanzania kupitia dira ya 2050 inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini.
“Tanzania imepiga hatua kubwa kijamii na kiuchumi kutokana na ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) wa kudumu tangu mwaka 2000, lakini viwango vya juu vya umasikini na uwekezaji mdogo katika kubadilisha kilimo cha kutegemea mvua vinaifanya nchi kuwa hatarini zaidi kwa athari za tabianchi,” amesema Nathan Belete, Mkurugenzi wa Nchi wa Benki ya Dunia.
“Kuunganisha masuala ya tabianchi katika mipango na utekelezaji wa maendeleo katika ngazi zote ni mkakati wa busara na wa kujivunia kwa Tanzania,” amesema.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema: “Serikali yetu inatambua kuwa mabadiliko ya tabianchi ni changamoto na pia fursa kwa mustakabali wa Tanzania. Hivi karibuni, tumeanzisha michango yetu ya kitaifa na mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo ni msingi thabiti wa njia endelevu zaidi.”
“Tunajitahidi kuwekeza kwa watu wetu na kuhakikisha jamii zilizo hatarini zaidi zinawezeshwa kukabiliana na changamoto za tabianchi, kwa sababu tunajua hatua hizi pia hufungua njia mpya za ukuaji endelevu zaidi,” amesema.