STRAIKA wa Singida Black Stars, Elvis Rupia juzi alifunga mabao mawili wakati timu hiyo ikiizamisha Dodoma Jiji kwa mabao 2-1, huku mwenyewe akisema ana imani anaweza kufanya makubwa zaidi kuliko sasa ili kuisaidia timu hiyo ikate tiketi ya mechi za kimataifa kwa msimu ujao.
Msimu uliopita Rupia aliionja michuano ya CAF akiwa na Singida Fountain Gate iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho na kucheza Kombe la Shirikisho Afrika, japo walitolewa raundi ya pili na Future ya Misri kwa mabao 4-2, huku yeye akifunga bao pekee kwa mchezo wa nyumbani.
Mabao mawili ya juzi yalimfanya Rupia kufikisha mabao saba akiongoza orodha ya wafungaji akimng’oa Seleman Mwalimu wa Fountain Gate ambaye jioni ya jana alikuwa uwanjani kupambana kurejea katika nafasi hiyo wakati wakivaana na Coastal Union.
Mkenya huyo takwimu zinaonyesha ameisaidia Singida kurejea katika wimbi la ushindi baada ya dakika 360 za kutokuwa na ushindi, huku mwenyewe akisisitiza wakati anazungumza na Mwanaspoti kuwa, yupo tayari kujitoa kwa asilimia 100 kwa ajili ya timu yake ili kufikia malengo yao ya kumaliza ligi katika nafasi nzuri.
Kabla ya mchezo huo, Singida ilikuwa katika presha kubwa ya matokeo baada ya kupoteza dhidi ya Yanga (1-0) na Azam (2-1), pia ikitoka sare na Tabora United (2-2) na Coastal Union (0-0), mwenendo ulioifanya ing’olewe kileleni mwa msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ushindi dhidi ya Dodoma Jiji umewafanya kufikisha pointi 27 sawa ilizonazo Yanga iliyopo nafasi ya tatu, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa Singida ikifunga 18 na kufungwa tisa wakati Yanga ikifunga 16 na kufungwa manne.
“Mchezo dhidi ya Dodoma ulikuwa mgumu, lakini tulipambana na kupata matokeo mazuri. Tunaamini tutafanya vizuri zaidi kadri msimu unavyoendelea,” alisema Rupia.
Rupia ambaye anashikilia nafasi ya juu katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu akiwa na mabao saba, amechangia asilimia 38.89% ya mabao yote ya timu yake, jambo linalothibitisha umuhimu wake katika safu ya ushambuliaji.
“Hii ni changamoto kubwa kwangu, lakini naamini nina uwezo wa kufanya zaidi. Timu yangu ina uwezo wa kufika mbali, na ni jambo la muhimu kuendelea kupigania nafasi ya juu katika msimamo,” aliongeza Rupia.
Rupia alipata mafanikio makubwa msimu wa 2022–23 wa Ligi Kuu ya Kenya, ambapo alikuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 27 akiwa na Kenya Police FC, na kuweka rekodi mpya kwa kuvunja ile ya miaka 47 iliyowekwa na Maurice Ochieng aliyefunga mabao 26 mwaka 1976.