Dar es Salaam. Maambukizi katika mfumo wa hewa, mkojo, malaria na magonjwa yasiyoambukiza ni miongoni mwa yaliyotajwa kusumbua Watanzania kwa mwaka 2024, huku wataalamu na wadau wa masuala ya afya wakisisitiza kuongezwa kwa jitihada katika utoaji wa elimu ya namna gani ya kuyaepuka.
Pia katika orodha iliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea inaonyesha kuwa magonjwa hayo yaliongoza katika mahudhurio ya wagonjwa wa nje hospitalini kuanzia Januari hadi Juni.
Januari 10, 2023 aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari alitaja magonjwa yanayotokana na maambukizi ya mfumo wa hewa pamoja na njia ya mkojo kuongoza kwa kuathiri watu wengi.
Alisema maambukizi ya mfumo wa hewa yaliwaathiri Watanzania 4,901,844, sawa na asilimia 18.9, huku matatizo ya njia ya mkojo (UTI) ikiathiri Watanzania 4,095,104, sawa na asilimia 15.8.
Septemba 2024, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) ilitoa takwimu za matukio muhimu 2023 ambazo ndani yake pia zilibainisha magonjwa 20 yaliyoongoza kwa vifo ambapo magonjwa ya mfumo wa upumuaji yaliongoza kwa asilimia 9.9 ya vifo vyote.
Wataalamu hao wamechambua sababu ya kuendelea kwa magonjwa hayo kusumbua na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mfumo wa upumuaji, Elisha Osati anasema magonjwa ya mfumo wa upumuaji yamekuwa yakiongezeka katika kipindi cha miaka minne mfululizo.
Anasema tangu kutokea kwa mlipuko wa Uviko-19, uliongeza shida ya upumuaji zaidi, ingawaje matatizo ya kupumua yamekuwa yakiongezeka miaka michache nyuma.
“Kumekuwa na nimonia za mara kwa mara zinazotokea kwa maana ya maambukizi ya njia ya hewa, kama kifua kikuu bado yapo tunapambana nayo, virusi wanaosababisha mafua pia. Kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa yametokea mabadiliko ya virusi na wanavyoshambulia kwa binadamu, lakini pia katika mfumo wa njia ya hewa,” anasema.
Dk Osati, ambaye pia ni mshauri na mtaalamu wa masuala ya afya, anasema mabadiliko tunayoyaona katika suala la mafua na maambukizi katika njia ya hewa yanatokana na mabadiliko ya hali ya hewa inayobadilisha wadudu tofauti, katika kupambana huko inasababisha madhara kwa viumbe vingine, ikiwemo binadamu.
“Haya maambukizi tunayaona kwa sababu ya mabadiliko na joto limekuwa jingi. Mahali pengine baridi imekuwa kali, lakini joto linasababisha hili kwa kiasi kikubwa, mabadiliko ya mazingira, hewa ya ukaa, hewa chafu imekuwa ikitoka kwa wingi kutoka kwenye viwanda, magari, mashine mbalimbali inasababisha uharibifu wa wadudu wanaoishi katika njia ya hewa na kusababisha wao kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Bakteria anaweza kutoka mdomoni kwenda kwenye koo kwa chini mpaka kwenye mapafu, kingine ni mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha hewa kuwa chafu hadi kuongeza maambukizi pamoja na pumu,” anasema Dk Osati.
Kuhusu magonjwa ya maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), Daktari wa magonjwa ya binadamu, Rachel Mwinuka anasema ni magonjwa ambayo yamekuwa yakisumbua haswa kwa upande wa wanawake.
Dk Rachel anasema ugonjwa huo husababishwa na bakteria na umekuwa ukiwapata wanawake zaidi kuliko wanaume kwa sababu kwa mwanamke njia ya urethra ‘mkojo’ ni fupi kuliko ya wanamume, hivyo uwezekano wa kupata maambukizi ni mkubwa zaidi.
Kutozingatiwa kwa usafi wa vyoo, kubana haja ndogo kwa muda mrefu, kutozingatia unywaji wa maji ya kutosha kwa siku, upakaji wa manukato na uwekaji wa vitu visivyohitajika katika sehemu za siri, hasa kwa wanawake anazitaja kama baadhi ya visababishi kupata maambukizi ya ugonjwa huo. Hata hivyo, alionya tabia ya baadhi ya watu kutumia dawa za kutibu UTI bila kwenda hospitali kufanyiwa vipimo na kupata ushauri wa daktari na kueleza kuwa tabia hiyo inaweza kutengeneza usugu wa dawa katika mwili.
Anasema ni vyema kuzingatia usafi ili kujikinga na ugonjwa wa UTI, hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira yanayowaweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni vyema kuhakikisha choo ni kisafi na kumwaga maji mengi kabla ya kukitumia.
“Vilevile ni vyema kwa wanawake kuhakikisha wanajiepusha na uwekaji au upakaji wa vitu katika sehemu za siri na kuhakikisha wanakunywa maji ya kutosha ili kuepuka kupata ugonjwa huo,” anasema Dk Rachel
Anasema pale mtu anapojihisi dalili za ugonjwa huo, ikiwemo kupata maumivu wakati wa kutoa haja ndogo, kutoa mkojo wenye rangi ya chai na harufu kali, homa, maumivu ya kiuno na nyinginezo ni vyema kuwahi hospitali kupatiwa tiba.
“Kuna baadhi ya watu wanapohisi tu dalili hukimbilia kunywa dawa bila ya kumuona mtaalamu wa afya, kufanyiwa vipimo na kupata ushauri, hii ni hatari, kwani inaweza kukufanya kutopata tiba stahiki ambayo itasababisha ugonjwa huo kujirudia tena au kutengeneza usugu wa dawa,” anaeleza Dk Rachel.
Daktari bingwa wa Fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili anasema ili kukabiliana na magonjwa hayo, ni muhimu jamii iendelee kupatiwa elimu na kukubali kubadili mtindo wa maisha.
“Jamii inapaswa kuacha mitindo isiyo bora ya maisha, kama vile unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara uliopitiliza, kutofanya mazoezi pamoja na ulaji mbovu,” anasema.
Dk Mashili anasema magonjwa yasiyoambukiza yana athari siyo tu kwa afya ya mtu binafsi, bali pia maendeleo ya Taifa na mikakati ya kufikia maendeleo endelevu (SDG’s).
“Bahati nzuri magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuzuilika endapo tutashirikiana kwa pamoja kuelimisha jamii zetu kwa usahihi ili waweze kufuata taratibu za ulaji zinazofaa, kufanya mazoezi pamoja na mtindo bora wa maisha kwa jumla,” anasema.