Dar es Salaam. Unaukumbuka wimbo wa Zuwena uliotamba miaka ya zamani na Bendi ya Dar International?
Katika wimbo huo, mwanamuziki Marijani Rajabu alikuwa anasimulia namna alivyopokea taarifa ya ajali iliyotokea katika eneo la daraja maarufu la Salenda, baada ya magari mawili kugongana na miongoni mwa majeruhi alikuwemo mpenzi wake, Zuwena.
Moja ya beti za wimbo ilisema:
“Ilikuwa asubuhi iii na mapema…. jua linachomoza….
Siku hiyo nilipatwa na mshtuko usiosemekana aaa …
Niliposikia habari kumetokea na ajali ya kutisha…
Kwenye daraja la Salenda, magari mwili yamegongana.”
Huwezi kutaja maeneo ya jiji la Dar es Salaam, ukaliacha daraja hili lililopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, zamani Bagamoyo. Daraja hilo linapita juu ya Mto Msimbazi, mahali ulipo mdomo wa mto huo unaomwaga maji baharini.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa daraja hilo, lililojengwa mwaka 1929 kabla ya Tanganyika kupata uhuru wake, limekuwa mojawapo ya alama muhimu za jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, mhifadhi historia kutoka Makumbusho ya Taifa, Shomari Shomari anasema jina la daraja hilo lilitokana na mzungu, John Einar Selander aliyekuwa mkurugenzi wa kwanza wa idara ya jamii na kazi katika Serikali ya Tanganyika.
Hivyo jina hilo lilitoholewa kutoka jina Selander hadi kuwa Salenda.
Hata hivyo, daraja linaloonekana kwa sasa na kutumika, ni matokeo ya uboreshaji uliofadhiliwa na Shirika la Misaada la Japani (JICA) mwaka 1982 kupitia kampuni ya ujenzi ya Kajima.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.