Dar es Salaam. Mwaka 2024 ulipoanza usafiri wa reli ya kati Tanzania, ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kadhaa.
Reli hiyo inayosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), inatumia mfumo wa reli ya zamani (MGR) uliojengwa wakati wa ukoloni.
Miongoni mwa changamoto ni kasi ndogo, hivyo kuchukua muda mrefu kwa abiria na mizigo kusafiri kati ya miji mikuu kama vile Dar es Salaam, Dodoma, na Mwanza.
Kutokana na reli hii kuwa ya zamani, kulikuwa kukijitokeza matatizo yaliyohitaji matengenezo ya mara kwa mara, huku pia kukiwa na matengenezo ya vichwa vya treni na mabehewa.
Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto nyingine, eneo la Godegode mkoani Dodoma limekuwa likikumbwa na tatizo kwenye miundombinu ya reli, hasa wakati wa msimu wa mvua.
Mafuriko mara kadha yamesababisha uharibifu wa tuta la reli, hivyo kuvuruga shughuli za usafiri jambo lililoathiri maisha ya wakazi wa eneo hilo na abiria kwa jumla.
Pamoja na changamoto hizo, reli hii ya zamani bado ilikuwa ikitumika kwa sababu ya gharama nafuu ukilinganisha na usafiri wa barabara au wa anga.
Serikali kupitia TRC katika kukabiliana na changamoto hizo, ilianza na inaendelea kutekeleza mradi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR).
SGR tofauti na MGR, ni suluhisho la muda mrefu la kuboresha usafiri, kuimarisha usafirishaji wa mizigo na kusaidia juhudi za kukuza uchumi wa Taifa.
Mfumo mpya wa SGR umeleta ufanisi kwa kupunguza muda wa safari, kuboresha usalama na kutoa huduma za kisasa kwa abiria na wafanyabiashara.
Juni 14, 2024 iliandikwa historia kwa kuanza safari ya SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro baada ya majaribio kadhaa yakiwamo ya Februari 27, 2024.
Agosti Mosi, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma.
Ndoto ya kuwa na mradi wa SGR ilianza kutekelezwa katika utawala wa rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.
Baada ya kifo cha Dk Magufuli Machi 17, 2021, Rais Samia alipokea kijiti cha urais, Machi 19, 2021 kipindi ambacho utekelezaji wa SGR ukiwa asilimia 22. Samia aliahidi kuendeleza miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake.
“Serikali yangu itaendelea kuendeleza mazuri yote yaliyoachwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli pamoja na kuleta mema mengine mapya,” alisema Rais Samia siku chache baada ya kuapishwa kuwa Rais.
Kwa mujibu wa TRC, ndani ya miezi minne limesafirisha zaidi ya abiria milioni moja kupitia treni ya SGR, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya waliokuwa wanasafirishwa na treni za zamani (MGR) kwa mwaka.
Taarifa iliyotolewa Novemba 20, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala ilisema:
“Shirika limefanikiwa kusafirisha abiria zaidi ya milioni moja katika kipindi cha miezi minne tangu uzinduzi wa njia za treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma Juni, 2024.
“Idadi hiyo ni mara mbili ya abiria waliosafirishwa na treni ya zamani (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja.”
Novemba 14, 2024 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Augustino Vuma akikagua mradi huo pamoja na wajumbe wengine, alisema zaidi ya Sh20 bilioni zimekusanywa tangu uanze.
“Tumeona katika taarifa zao TRC wametueleza hadi sasa zaidi ya Sh20 bilioni zimekusanywa tangu imeanza kutoa huduma za kusafirisha abiria kupitia treni ya kisasa ya SGR.
“Mapato yatokanayo na abiria huwa ni asilimia ndogo lakini asilimia 80 na zaidi mara nyingi inatokana na usafirishaji wa mizigo, kama haya yaliyopatikana ni asilimia 20 tunaamini mizigo ikianza wafanyabiashara wengi watatumia fursa hiyo na mapato ya shirika yataongezeka,” alisema.
Wakati idadi ya abiria ikiendelea kuongezeka, TRC Novemba 15 ilieleza utengenezaji wa mabehewa 264 ya mizigo nchini China umekamilika na yataletwa nchini Desemba hii.
Mabehewa hayo ni sehemu ya 1,430 ambayo yatatengenezwa na kampuni ya CRRC kwa mujibu wa mkataba.
Hakuna maendeleo yasiyo na changamoto. Mapinduzi katika usafiri wa reli yaliyoshuhudiwa mwaka 2024 yameathiri sekta zingine za usafirishaji.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimekuwa kikieleza kilio cha kupungua abiria wanaosafiri kwa njia ya barabara.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Taboa, Mustapha Mwalango aliieleza Mwananchi baadhi ya wamiliki, wamelazimika kuegesha mabasi kutokana na kukosa abiria.
SGR inatumia takribani saa tatu na dakika ishirini kusafiri kati ya Dar es Salaam na Dodoma, wakati umbali huohuo unachukua hadi saa 10 kwa basi.
Hata hivyo, wenye mabasi wameanzisha safari katika njia mpya ili kuendelea na biashara.
Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara wa Latra, Johansen Kahatano alikiri kuwa biashara ya mabasi imeporomoka.
Alisema uchunguzi kwa njia ya Dar es Salaam-Morogoro uliofanywa na Latra, ulibaini idadi ya abiria waliokuwemo kwenye mabasi nayo imepungua kwa asilimia 20.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude alisema usafiri wa reli ya kisasa ni mtandao muhimu kwa uchumi wa Tanzania.
Mkude alieleza licha ya mradi huo kuchelewa, umeanza kuleta matokeo chanya, akibainisha idadi ya abiria imekuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
TRC imeripoti kusafirisha zaidi ya abiria milioni moja tangu kuanzishwa kwa usafiri wa reli, jambo ambalo ni la kipekee kwa mradi wa aina hii.
Mkude alisema wingi wa abiria kwenye treni ya SGR, ni tafsri tosha kuwa Watanzania wameupokea mradi huo kwa furaha.
Alisema kutokana na ubora wa huduma za usafiri, safari ya Morogoro ilichukua saa tatu hadi nne kwa basi kutokea Dar es Salaam, lakini sasa inachukua saa 1.40 pekee.
“Kwa kweli, usafiri wa treni ni bora kwa abiria kwa sababu unasafirisha kwa haraka na bila foleni. Hii inaongeza ubora na uzoefu wa abiria. Sidhani kama watumiaji watakuwa na maumivu kwa sababu bado kuna mbadala wa kutumia mabasi kwa wale wanaopenda gharama za chini,” amesema.
Mkude amesema mradi wa SGR utatoa fursa kwa wafanyabiashara wa mabasi na malori kubuni biashara mpya zinazozingatia mahitaji ya sasa.
Amesema sekta binafsi inapaswa kubuni njia bora zaidi za kufanya biashara kulingana na mabadiliko ya soko.
Mtaalamu wa usafiri, Thomas Gowele, alisema usafiri wa reli utaleta faida kubwa kwa uchumi, hasa kwa mlaji wa mwisho, kwani utapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa.
Alisema nishati inayotumika kwenye treni ni umeme, ambao ni nafuu ukilinganisha na mafuta kwa malori.
“Wamiliki wa malori wataathirika, lakini usafiri wa reli utaongeza usalama na kupunguza ajali. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba watu 7,639 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani kutoka 2019 hadi Mei 2024,” alisema Gowele.
Katika kipindi hicho, ajali za barabarani zilizotokea zilikuwa 10,093 na majeruhi walikuwa 12,663, miongoni mwao wakipata ulemavu wa kudumu.
Gowele alisema zipo fursa zinazoonekana na zisizoonekanaza endapo treni ya mizigo itaanza, akisisitiza maeneo yote zitakapowekwa stesheni yatakuwa na mabadiliko makubwa ya biashara na makazi ya watu yataanzishwa.
Alisema ujio wa SGR katika sekta ya usafirishaji wa abiria na mizigo, ni hatua muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
“Ingawa wamiliki wa mabasi na malori wanaathirika, bado kuna fursa mpya ambazo zinahitaji kuzingatiwa. Ufanisi wa mradi huu utategemea ushirikiano kati ya sekta binafsi, Serikali na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa faida zinazopatikana zinatumiwa vyema,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta alisema hawatarajii ujio wa treni ya mizigo, kupunguza malori katika matumizi ya barabara.
“Lengo la ujenzi wa reli na matengenezo ya bandari ni kuongeza mzigo, hivyo tunategemea ongezeko la vyanzo vya usafirishaji,” alisema.