LILE sakata la Aisha Mnunka na klabu yake limepatiwa ufumbuzi baada ya pande hizo mbili kukutanishwa katika kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kilichokuitana jana Jumatano kuamriwa wakae meza moja kuyamaliza.
Agosti Mosi, mwaka huu, Mwanaspoti iliripoti nyota huyo wa timu ya taifa (Twiga Stars) alitoroka kambini ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya taifa.
Hata hivyo, baada ya sakata hilo, baadae Simba Queens ilitoa ripoti nyota huyo aliondoka kambini bila ruhusa na wamepeleka kesi Shirikisho la Soka nchini (TFF) juu ya kutoonekana klabuni kwa mchezaji wao.
Iko hivi. Mnunka baada ya kumalizana na majukumu ya timu ya taifa, Twiga StarsĀ hakurejea kambini wakati timu hiyo ikiwa inajiandaa na michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa wanwake ukanda wa CECAFA yaliyoanza Septemba.
Baada ya ukimya wa muda mrefu klabu hiyo ilianza kumtafuta kwenye simu yake lakini hakupatikana, Simba haikuishia hapo ikatangaza kwa umma kuwa mchezaji wao ametoroka ikidaiwa kuwa amefichwa na moja ya timu zinazoshiriki Ligi ya Wanawake (WPL).
Ukimya wa mchezaji huyo uliwafanya Simba wakimbuilie TFF kushtaki juu ya utoro wa mchezaji wao ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja unamalizika msimu huu.
Kesi hiyo iliyosikilizwa na wajumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kupitia kwa Mwenyekiti Said Soud, imeamuru mchezaji kukaa na Simba ili zimalizane juu ya sakata hilo.
Viongozi wa Simba na Mwanasheria wa mchezaji huyo waliohudhuria kesi hiyo kwa ajili ya shauri hilo, waliliambia Mwanaspoti kwamba bado hakuna uamuzi wa mwisho.
“Sisi Simba tulikuwa ndio walalamikaji na upande wa mchezaji wameomba tukae tuzungumze hivyo kamati imetoa nafasi kwao tujadili kwa pamoja,” alisema mmoja wa viongozi wa Simba Queens na kuongeza
“Mchezaji amevunja mkataba na timu kwa hiyo sisi kama timu tumekubali kumpokea na kumsikiliza na kikao kitakachofuata itakuwa Januari ambacho kitatoa majibu baada ya sisi kufanya mazungumzo.”