Morogoro. Licha ya kupoteza matumaini ya kuendelea na safari ya elimu kutokana na sababu mbalimbali, baadhi ya wasichana mkoani Morogoro wamepata mwanga wa kuzifikia ndoto zao.
Hiyo ni baada ya Shirika lisilo la kiserikali za Camfed kuwaendeleza kielimu kwa wale walioishia njiani, huku waliofeli wakipelekwa kupata elimu ya ufundi.
Wasichana hao ni wale walioshinda kuhitimu ngazi mbalimbali za elimu kutokana na ujauzito, umasikini wa familia na sababu nyinginezo.
Catherine Mtewele wa Ifakara ni miongoni mwa wanafunzi hao, anayesema ujauzito ulikatisha safari yake ya elimu akiwa kidato cha pili.
“Kwanza nilifeli mtihani wa kidato cha pili na kufeli kwangu kulitokana na umasikini kwenye familia yetu. Sikuweza kupata mahitaji na nikiwa mtaani ndipo nilipopewa mimba na mwanaume ambaye baadaye alinikimbia na kuniacha nahangaika na mtoto,” anasema.
Katikati ya mazingira hayo, anasema alikutana na maofisa wa Camfed waliomfadhili masomo katika chuo cha Veta Mikumi alikosomea ufundi wa kuchomelea.
Ufadhili haukuishia hapo, kwa mujibu wa Catherine, uliendelea hadi kupewa mtaji uliomwezesha kufungua ofisi ya kuchomelea na sasa ameajiri vijana wenzake wawili.
“Hili Shirika la Camfed lilipokuja kunifadhili waliniuliza kama naweza kuendelea na masomo ya sekondani au fani, mimi nilichagua kujifunza ufundi,” anasema.
Akieleza namna jamii inavyomchukulia kutokana na kazi yake hiyo, anasema mwanzoni watu walikuwa wakimuona binti wa ajabu huku wengine wakimbeza.
“Kuna watu walikuwa wakinikatisha tamaa na wengine wakinicheka kwa kuniambia hii kazi haitanifaa ya kiume na kwamba nitakomaa viungo, lakini mimi sikujali niliendelea kusimamia ndoto zangu mpaka leo nimekuwa ni fundi mkubwa Ifakara,” amesema.
Kwa sababu muda mwingi anakuwa kazini, anasema mama yake mzazi ndiye anayemsaidia kumlea mwanawe, lakini wakati mwingine analazimika kwenda kazini na mtoto.
Kutokana na kazi hiyo, Catherine anasema kwa sasa anamiliki nyumba ya vyumba viwili anayoishi na mama yake mzazi.
“Hivi karibuni nilipata zabuni kutoka Halmashauri ya kutengeneza madawati ya shule ya sekondari, fedha nilizopata nimemnunulia mama yangu jokofu kwa ajili ya kugandisha barafu na kuuza maji na juisi,” anasema.
Kuhusu baba wa mtoto, anasema alishakimbia mapema baada ya kumpa ujauzito, hivyo malezi ya mwanae limebaki kuwa jukumu lake pekee.
Mkurugenzi wa shirika la Camfed, Nasikiwa Duke amesema ni kiu ya shirika hilo kuhakikisha linafufua ndoto zilizofutika kutoka kwa mabinti mbalimbali nchini.
Anasema tayari walishakutana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kujadili namna ya kuwasaidia wasichana hao.
Anamwelezea Catherine kama binti wa mfano hasa kwa mabinti waliokata tamaa.
“Kupitia Shirika letu pia tumekuwa tukienda kwenye jamii za kifugaji ambazo mila na desturi zao zinawakandamiza watoto wa kike na kukatishwa ndoto zao kwa kuwaozesha wakiwa na umri mdogo.
“Tunashirikiana na Serikali kuzungumza na viongozi wa jamii hizo na kuwabadilisha mtazamo,” anasema.