Siri maambukizi ya VVU Kigoma kupungua

Kigoma. Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Kigoma yanatajwa kupungua kutoka asilimia 3.4 mwaka 2013 hadi 1.7 mwaka 2023 sawa na upungufu wa asilimia 50.

Takwimu hizo zimetolewa leo Ijumaa Desemba 13, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Matunzo wa Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wa ‘Afya Hatua’, Dk Frederick Ndossi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dk Redempta Mbatia.

Dk Ndossi ametoa takwimu hizo kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki 40 kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, zitakazosaidia kuratibu huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukwimi (Waviu) mkoani Kigoma.

Amesema kupungua kwa maambukizi ya VVU na kuongezeka kwa mwamko wa Waviu kujiunga na huduma za tiba na matunzo mkoani humo, ni matokeo ya jitihada za THPS kwa kushirikiana na wadau na Serikali kujenga uelewa, mazingira na mwamko wa jamii.

“Hivi sasa, wapokea huduma wengi wana afya nzuri na wanaendelea kujenga taifa letu kupitia shughuli mbalimbali. Isingekuwa uwepo wa matibabu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, wengi wangekuwa muda mwingi wako vitandani wakiugua magonjwa,” amesema Dk Ndossi.

Kuhusu pikipiki hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh141 milioni, Dk Ndossi amesema zimetolewa kupitia mradi wa ‘Afya Hatua’ unaotekelezwa na THPS kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (Pepfar) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC).

Amesema zitasambazwa kwenye vituo na kliniki za tiba na matunzo ya VVU katika halmashauri za Buhigwe (5), Kakonko (4), Kasulu (9) Kibondo, Kigoma (2) na Uvinza (11).

“Pikipiki hizi zinalenga kuwezesha huduma muhimu zinazohusiana na VVU, ikiwa ni pamoja na kusafirisha sampuli za kipimo cha wingi wa Virusi vya Ukimwi (HVL) hadi kwenye maabara,” amesema Dk Ndossi.

Pia amesema zitawezesha ufuatiliaji wa wateja waliokosa kuhudhuria katika kliniki na kuhimiza ufuasi wa huduma, kufuatilia ripoti na mawasiliano ya washirika wa ngono ili kuwawezesha kufikiwa na huduma za upimaji wa VVU na kusaidia huduma za kijamii kama vile usambazaji wa dawa za kupunguza hatari ya maambukizi ya VVU (PrEP) na uhamasishaji matumizi ya kondomu.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo, Andengenye amewataka watoa huduma ya afya kwenye vituo vya tiba na matunzo mkoani humo kuzingatia lengo la kukabidhiwa msaada huo huku akionya watakaozibadilishia matumizi hawatofumbiwa macho.

“Lengo la pikipiki hizi ni kujenga mazingira rafiki ya utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu waishio na VVU, hivyo basi niwatake watoa huduma mzitumie kuwafikia wanyonge ambao wanahitaji kufikishiwa huduma na hawana uwezo wa kufika katika vituo,” amesema Andengenye.

Kauli ya Andengenye imeungwa mkono na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Damas Kayera kuwa anaamini baada ya watoa huduma ya afya kukabidhiwa pikipiki hizo, watapambana na kupunguza maambukizi ya VVU mkoani humo kutoka asilimia 1.7 ya sasa hadi asilimia sifuri (0) ifikapo 2030.

Related Posts