TADB yaingia mkataba na Mchongo TV kuhamasisha kilimo

Na Imani Nathaniel, Mtanzania Digital

Katika kukuza sekta ya kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imeingia mkataba wa makubaliano wa ushirikiano kwa lengo la kuchochea mapinduzi ya kilimo, uvuvi, mifugo.

Tukio la utiaji saini limefanyika Desemba 12, 2024 katika Makao Makauu ya TADB Dar es Salaam, huku makubaliano hayo yakijikita pia katika sekta fungani kama ardhi, biashara na maendeleo, maji na fedha katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Akizungumza katia hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Banki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB, Frank Nyabundege, amesema kuwa chaneli hiyo inalenga kuhamasisha ukuaji wa sekta hizo muhimu.

” Katika utafiti wetu tumegundua kuwa changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa taarifa sahihi kwa wakati na kushindwa kufikia ubora wa viwango katika masoko ya kimataifa ambapo sasa mchongo Tv itakuwa jukwaa la kipekee litakalotoa taarifa za masoko duniani na kuibua fursa mpya kwa kila rika,”amesema Nyabundege.

Aidha amesema kituo hicho kitalenga katika vipindi vya kuelimisha jamii juu ya matumizi ya teknolojia katika kilimo ,ufugaji na uvuvi wa kisasa na endelevu pia taarifa za hali ya hewa ,ushauri juu ya upatikanaji wa mikopo ya kilimo na njia bora za kuimarisha ufungaji bidhaa kwa masoko ya ndani na nje na kutarajia kuwa sehemu ya mapinduzi ya kijani Tanzania.

Amesema benki hiyo inalenga inalenga kuimarisha uzalishaji wa kilimo kwa wakulima wadogo , kukuza kilimo cha kibiashara na kuongeza thamani ya mazao, kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa wakulima na wazalishaji pamoja na kuhakikisha kilimo kinachangia zaidi katika ukuaji wa uchumi nchini.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mchongo TV, Juhayna Kusaga, amasema kuwa makubaliano yaliyosainiwa ni chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo ambapo watanzania watarajie kupata ujuzi mbalimbali kupitia vipindi vinavyoenda kurusha.

” Watanzania ni wakati wetu sasa tuamke na tukumbuke pia biashara ya kilimo ili tuweze kujikwamua na kuleta maendeleo nchini kupitia fursa na mikopo ya kilimo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo huku tukifuatilia elimu mbalimbali zinahusisha maswala mazima ya kilimo kupitia televisheni iliyowashwa sasa”, amesema.

Related Posts