MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar
Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne zijazo (tarehe 13 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo leo Desemba 12, 2924 imeeleza, kwa sasa, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini.
Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati ya tarehe 14 na 16 ya Disemba 2024.
USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.