TRA YAZINDUA BOTI YA DORIA ZIWA VICTORIA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Boti ya doria ambayo itatumika kupambana na magendo katika Ziwa Victoria na kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi ambavyo vimekuwa vikifanywa na watu wasioitakia mema Taifa la Tanzania.

Uzinduzi wa Boti hiyo ya Doria umefanywa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe Hamad Chande mkoani Mwanza na kueleza kuwa ujio wa Boti hiyo ya kisasa utakomesha magendo yanayofanyika katika Ziwa Victoria.

Mhe. Chande amesema kila Mtanzaia kwa nafasi yake anapaswa kupambana na magendo maana yanaliumiza Taifa Zima na siyo TRA kama wengi wanavyodhani maana kodi wanayokwepa wafanya magendo, ingeweza kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda amesema Magendo yanayofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu yamekuwa yakichangia kuharibu Uchumi wa Nchi, kuhujumu Biashara za wengine, kuchochea uhalifu na kuharibu usalama wa Nchi, hivyo Boti ya Doria iliyozinduliwa itakomesha vitendo hivyo.

Amesema Boti ya Doria iliyozinduliwa jijini Mwanza, itapambana na magendo na kuokoa mapato yaliyokuwa yanapotea kutokana na ukwepaji kodi kupitia bidhaa za magendo.

“Miongoni mwa magendo makubwa yanayoingi kupitia Ziwa Victoria ni vipodozi ambavyo mbali na kukwepa kodi vimekuwa vikiharibu afya za wananchi na kazi yetu siyo tu kudhibiti tu mapato, pia tunaangalia afya za watanzania” Amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema walipakodi wa Tanzania wanataka kuwepo na usawa katika kodi hivyo kuzinduliwa kwa Boti hiyo kunatekeleza matakwa ya wananchi maana kwa kuzuia magendo kutakuwa na usawa wa biashara kwa kila mtu kulipa kodi.

“Usawa wa biashara unakosekana maana unakuta mtu aliyeingiza bidhaa za magendo anaziuza kwa bei ya chini kuliko wenzake maana hajazilipia kodi, sasa tutahakikisha wote wanalipa kodi” Bw. Mwenda

Kamishna Mkuu Mwenda amesema Magendo yanayofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu yamekuwa yakichangia kuharibu Uchumi wa Nchi, kuhujumu Biashara za wengine, kuchochea uhalifu na kuharibu usalama wa Nchi, hivyo Boti ya Doria iliyozinduliwa leo mkoani Mwanza itakomesha vitendo hivyo.

Ameeleza kuwa TRA itatoa motisha kwa mwananchi yeyote atakayefichua watu wanaojihusisha na magendo au wanaokwepa kodi na kuwa suala la motisha lipo kisheria.

Naye Kamishna wa Forodha Bw. Juma Hassan amesema Boti hiyo ya kisasa ina mwendo wa kasi ya kutosha kupambana na magendo na kuwa ni Boti ya tatu kukamilika huku Boti ya 4 ikiwa bado ipo kwenye hatua za kutengenezwa.

Amebainisha kuwa Boti hiyo itakuwa ni ya kufunika na ndani yake itakuwa na vitanda 3 pamoja na sehemu ya kupikia ambayo itaiwezesha kukaa majini muda mrefu na matengenezo yake yanagharimu milioni 865.1 huku Boti za wazi ikiwemo iliyozinduliwa leo zikigharimu Bilioni 1.6 Sawa na Sh. Milioni 530 kwa kila Boti.

Kwa upande wa mkoa wa Mwanza Uongozi wa mkoa huo kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema wanashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuilinda Boti ya Doria iliyozinduliwa kwaajili ya kufanya Doria katika Ziwa Victoria.

Amesema mkoa wa Mwanza umekuwa ukikusanya mapato mengi na kushika nafasi ya pili kwa makusanyo jambo ambalo limewapa motisha baada ya kupatiwa zaidi ya Sh. Trilioni 5 za miradi ya maendeleo.


















Related Posts