Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam, wameshiriki warsha ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati) ya kukuza taaluma na kufanya ziara ya kiwanda cha umeme iliyoratibiwa na GE Vernova kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Tukio hili lilifanyika katika mazingira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chenye zaidi ya wanafunzi 35,000, wengi wao wakiwa wanajifunza masuala ya uhandisi na taaluma nyingine za STEM. Hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha uwezo wa kitaifa katika maeneo haya muhimu.
Tukio hilo la siku moja liliwapa wanafunzi nafasi ya kukutana moja kwa moja na wataalamu kutoka GE Vernova na TANESCO. Kupitia mawasilisho na mijadala ya maswali na majibu, wanafunzi walipata uelewa wa programu za uhandisi zinazochochea taaluma katika sekta ya nishati, pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana. Mada zilizojadiliwa zilihusisha mabadiliko ya nishati, athari za mabadiliko ya tabianchi, na mchango wa TANESCO katika kupanua upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Pia, kulikuwa na mjadala wa paneli uliowajumuisha wataalamu kutoka GE Vernova, TANESCO, Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC), na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Jopo hilo liliwaelezea wanafunzi safari za kitaaluma za washiriki wake na fursa zinazowangoja wahitimu wa STEM katika nyanja zao za kazi.
“Umeme wa uhakika na wenye ufanisi ni nguzo muhimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. TANESCO imejizatiti kujenga miundombinu inayohitaji ujuzi wa kitaalamu wa ndani na vipaji vya kihandisi,” alisema Renata Ndege, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mipango, Utafiti na Uwekezaji, TANESCO. “Programu kama hizi ni muhimu sana kufanikisha malengo yetu,” aliongeza.
“GE Vernova imejizatiti kuchangia kikamilifu mabadiliko ya nishati Tanzania,” alisema Oluwatoyin Abegunde, Mkurugenzi Mtendaji wa Aeroderivatives, Gas Power wa GE Vernova. “Kwa kutumia teknolojia zetu za hali ya juu, tumejipanga kusaidia wateja wetu kujenga mfumo endelevu na imara wa nishati. Kwa kushirikiana na TANESCO na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tunalenga kuwapa wanafunzi uelewa mpana wa fursa za kitaaluma zinazohusiana na sekta ya nishati pamoja na nafasi za kielimu. Wahandisi wachanga wa STEM ni muhimu katika kuunda mfumo wa nishati unaozingatia ustahimilivu, upatikanaji, na uendelevu,” aliongeza.
Dkt. Aviti, Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Uhandisi wa Umeme, Chuo cha Uhandisi na Teknolojia, alisema: “Katika chuo chetu, tunatoa mafunzo ya kiutendaji na kinadharia. Matukio kama haya yanawasaidia wanafunzi kuona jinsi masomo yao yanavyotumika katika hali halisi ya maisha.” Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na taasisi za elimu ni muhimu katika kuhakikisha wahitimu wanachangia maendeleo ya sekta ya nishati nchini Tanzania na kufanikisha malengo mapana ya kitaifa.
Kwa zaidi ya miaka 130, GE Vernova imekuwa ikichangia katika mnyororo wa thamani ya umeme Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikijumuisha uzalishaji wa umeme wa upepo, maji, na gesi, pamoja na usafirishaji, usambazaji, na programu suluhishi zinazoboresha uzalishaji wa nishati. Hapa Tanzania, teknolojia za GE Vernova zinachangia kwa kiwango kikubwa katika usambazaji wa umeme wa taifa, ikijumuisha takriban megawati 600 (MW) za mitambo ya gesi, ikiwemo Ubungo III (92 MW), Kinyerezi I (150 MW) na Kinyerezi I Extension (150 MW).