Vyama vya siasa kufungua pazia maoni Dira ya Taifa 2050

Dar es Salaam. VyamaĀ  19 vya siasa vilivyosajiliwa nchini Tanzania vinatarajiwa kufungua pazia la utoaji wa maoni kuhusu Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyozinduliwa Desemba 11, 2024, Zanzibar.

Vyama hivyo vinaanza kutoa maoni kesho Desemba 14, 2024, huku matarajio ya wananchi kwa Dira hii yakiwa ni kujenga uchumi imara, unaostawi na kuboresha maisha yao.

Pia, wanatarajia huduma bora za jamii ikiwemo elimu na afya, utawala bora, utoaji haki, ulinzi na usalama, maendeleo ya teknolojia na ubunifu, pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.

Mchakato wa kuandika Dira hii ulianza Aprili 2023 chini ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango. Waziri wa Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema leo Desemba 13, 2024, kuwa vyama vya siasa vimeshapokea rasimu ya dira hiyo kwa ajili ya kuisoma kabla ya kutoa maoni yao.

“Wadau wameshaiona dira na maudhui yake, sasa kinachofuata ni maoni kuhusu walichokiona na wanachotamani kiboreshwe. Kesho vyama vya siasa 19 vimealikwa kutoa maoni yao,” alisema Profesa Mkumbo.

Aliongeza kuwa, Desemba 15, 2024, Chama cha watu wenye ulemavu kitatoa maoni yake kutokana na masuala yao kujumuishwa katika rasimu. Jumatatu, Desemba 16, wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari watatoa maoni yao, ikifuatiwa na sekta ya fedha Desemba 17.

“Ukusanyaji wa maoni utakamilika Januari 12, 2025, ili wataalamu waweze kukamilisha rasimu ya pili itakayopokewa Januari 18 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Baadaye itajadiliwa na serikali, Baraza la Mawaziri, Tume ya Mipango, na kuwasilishwa bungeni kati ya Aprili na Mei 2025 kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa Dira kamili,” alisema.

Hadi sasa, serikali imekusanya maoni ya wananchi milioni 1.17 kupitia tafiti katika kaya 15,483, ujumbe wa simu (USSD) 1,118,978, tovuti 13,459, na makongamano 12 yaliyohudhuriwa na watu 22,779.

Pia, kulikuwa na mahojiano na viongozi waliopo madarakani na wastaafu 44, mikutano ya semina 220, na nyaraka 33 zilizokusanywa.

Related Posts