Wababe wa Yanga watambiana Tabora

Timu za Tabora United na Azam FC ambazo ndio timu pekee zilizoifunga Yanga kwa msimu huu zimetambiana kueleeka mchezo wa Ligi kuu bara utakaochezwa leo Desemba 13, 2024 kila mmoja ikijinasibu kufanya vizuri katika mchezo huo utaakopigwa Alsan Mwinyi mkoani Tabora.

Akizungumza na Mwanaspoti Kocha wa Tabora United mwenyeji wa DR Congo Anicet Makiadi amesema kuelekea mchezo huo timu yake imejiandaa vyema licha ya changamoto lukuki ndani ya timu yake.

“Maandalizi yetu kueleeka mchezo dhidi ya Azam yako vizuri, tumekuwa na muda wa kupumzika baada ya mchezo wetu uliopita dhidi ya KMC lakini nathubutu kusema tuko tayari kwa mchezo, hapo nyuma tulipata matatizo kidogo ndani ya timu ambayo yaliathiri maandalizi yetu lakini hilo halituumizi kichwa kwani bado tunaendele ana mpango wetu wa kupata matokeo” amesema Makiadi

Aidha Makiad amesema mchezo dhidi ya Azam utakuwa mgumu kutokana na kiwango bora kinachoonyeshwa na Azam fc hasa baada ya ujio wa kocha mpya lakini anaamini nguvu wanayopewa na mashabiki wa timu hiyo itawasaidia kupata matokeo katika mchezo huo muhimu.

Katika hatua nyingine Kocha huyo amesema katika kipindi ligi ilipokuwa imesimama alitumia muda mwingi kuongeza ujuzi kwenye safu yake ya ushambuliaji kwakua imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi na kushindwa kupata mabao inavyotakiwa hivyo amesema anaamini timu yake itaanza kufunga mabao mengi katika kila mchezo.

Kocha mkuu wa Azam Rachid Taoussi amesema kuelekea mchezo dhidi ya Tabora atawaheshimu zaidi wapinzani wao kwakua Tabora United ni timu kubwa.

“Kuelekea mchezo wetu na Tabora tunaamini utakuwa mchezo mgumu, tumeandaa mbinu zetu kuelekea huo mchezo lakini tunategemea ushindani mkubwa, kwanza uwanja utakuwa tofauti na ule tuliozoea lakini hilo  halitatuzuia kupatambana kupata ili kufanikisha azma yetu” amesema na kuongeza

“Nimezungumza na wachezaji tumejianda kisaikolojia kwenye huu mchezo kwani tunatakiwa kushinda kila mchezo kama mnavyoona Tabora imekuwa na kiwango bora kwenye michezo yake hivyo mpaka kufika hapa tumejiandaa na tunaitaka mechi” amesema

Katika michezo mitano ya mwisho timu ya Azam imepata matokeo katika michezo yote huku Tabora wenyewe wakishinda michezo mine pekee na kutoka sare moja katika michezo yake mitano ya mwisho waliyocheza hivi karibuni.

Mpaka sasa Azam FC wako nafasi ya kwanza  kwenye msimamo wa Ligi kuu bara baada ya kucheza mechi 13 na kukusanya alama 30 huku Tabora United weneywe wakicheza mechi 13 na kukusanya alama 21 huku wakiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Related Posts