Wavuvi Ziwa Victoria wajadili matumizi ya ‘drone’ kudhibiti uvuvi haramu

Mwanza. Baadhi ya wavuvi katika Ziwa Victoria wamesema bila usimamizi wa sheria na uwajibikaji, ndege zisizo na rubani (drones) haziwezi kumaliza uvuvi haramu na kutunza viumbe maji katika ziwa hilo.

Wavuvi hao wameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 13, 2024 zikiwa ni siku chache baada ya Mkurugenzi wa Uvuvi, Profesa Mohamed Sheikh kuwaambia wadau wa uvuvi kuwa mwaka wa fedha ujao (2025/26), Serikali ina mpango wa kutumia ndege hizo kufanya doria.

Alisema kwa Ziwa Victoria itaanza na drones mbili ili kutokomeza uvuvi haramu na kuhakikisha kunakuwa na usalama wa viumbe maji.

Profesa Sheikh alizungumza na wadau hao kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe katika mkutano wa kupokea maoni ya kuboresha kanuni za uvuvi, uliofanyika Nyakahoja jijini Mwanza Desemba 2, 2024.

Mvuvi katika mwalo wa Mswahili, Hamis Mtumwa amesema njia pekee ya kukomesha uvuvi haramu na kulinda mazalia ya samaki ni kuhakikisha sheria na kanuni za uvuvi zinafuatwa.

“Kuna boti zinafanya doria ziwani, nini tija yake? Uvuvi haramu si bado upo? Tena naona kama ndio unaongezeka…kwa nini licha ya maofisa uvuvi na boti za doria za kisasa kuwepo lakini bado kuna baadhi yetu wanavua isivyotakiwa? Kwa sababu hakuna anayefuata sheria na kanuni,” amesema.

Akiwa na mtazamo kama huo, Katibu wa Chama cha Wavuvi nchini (Tafu), Jephta Machandaro amesema japo hawajui ufanisi wa ndege hizo, lakini wanaamini siku sheria za uvuvi zikiwa na meno na kufanya kazi, mazao ya samaki ziwani yatalindwa na ndio utakuwa mwisho wa uvuvi haramu.

“Kanuni zinaruhusu nyavu haramu kuwa majini? Hapana. Kanuni inaruhusu kuvua samaki wachanga, watu kuwauza na kuwanunua? Hapana. Sasa mbona samaki hawa wanapatikana kila maeneo mtaani muda wote? haya yanafanyika mchana kweupe kila eneo, sasa hizo drone zenyewe zikija zitamchukulia mtu hatua gani?

“Ofisa uvuvi yupo, polisi yupo, lakini hayo mambo yanatendeka, sasa hizo drones zitafanya nini? Hatujui,” amesema Machandaro.

Amehoji kama ambavyo Serikali imefanikiwa kudhibiti majangili, imeshindwaje kudhibiti wavuvi ambao hawana silaha huku akiongeza kuwa ni uamuzi tu iwapo itaamua kuwadhibiti, itadhibiti uvuvi haramu.

“Labda kuna mnyororo wa wanufaikaji ndio maana imeshindikana kuwadhibiti…lakini Serikali ikiamua kuwadhibiti inawadhibiti tu kwa kushirikiana na wananchi,” ameeleza Machandaro.

Hata hivyo, mchuuzi wa mazao ya samaki mkoani Mwanza, Aisha Madhili amesema ndege hizo zinaweza kuwa na msaada mkubwa endapo rushwa itadhibitiwa hasa kwa wasimamizi wa sheria kwenye mialo ya uvuvi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tafu, Bakari Kadabi amesema: “Kwanza drones ni kitu ambacho sisi hatukijui na kama vitu ambavyo hatuvijui, hatujui ufanisi wake. Sidhani kama ndege inaweza kuona nyavu haramu au ikachambua huyu ni mvuvi haramu, tunaomba tupewe elimu ya ufanisi wa drones katika eneo hili.”

Amesema kanuni ya uvuvi wa dagaa kuanzia mita 500 kutoka kwenye fukwe ifuatwe ili kuokoa mazalia ya samaki kwa kuwa wavuvi wengi wanavua ndani ya mita hizo, wanavua hadi watoto wa samaki.

Ametaja njia ya kumaliza uvuvi haramu ni Serikali kuhakikisha zana haramu haziingii nchini kwa kuwa yenyewe ndio inatoa vibali, vya zana hizo kuingia lakini pia iweke mpango mzuri sababu hata wanaouza nyavu wanauza kwa vibali.

“Wote wanauza kwa vibali, waagiza nje wanapewa kibali na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ndio nyavu zinaingia, maana yake nini sasa? Kama zinaingia nyavu na nyavu haramu zinaingia inamaanisha kuna mapungufu ya uwajibikaji,” amesema Kadabi.

Katika Ziwa Victoria, kuna aina sita za uvuvi haramu ambazo ni uvuvi wa gizagiza ambao unafanyika bila wahusika kutumia taa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Uvuvi haramu wa kumbakumba ambao baadhi ya wavuvi wanatumia nyavu halali za dagaa za milimita nane kandokando ya ziwa yaliko mazalia ya samaki na hivyo kunasa samaki wachanga hadi mayai.

Uvuvi mwingine  haramu wa machoteni ambao hutumia makokoro ya kawaida yanayoruhusiwa kisheria lakini wahusika hutumia ujanja wa kutia nanga katikati ya maji na kuvutia kokoro badala ya kufanya hivyo wakiwa nchi kavu ufukweni.

Uvuvi haramu wa timba ambao wavuvi wanatumia nyavu zisizoonekana kirahisi zinazodaiwa kutengeneza kemikali hatarishi zinapogusana na samaki na uvuvi haramu wa manyamunyamu unaotumia nyavu za kokoro zenye vipimo visivyoruhusiwa kuvulia dagaa.

Related Posts