Waziri Masauni Aahidi Kuongeza Kasi Katika Utekelezaji wa Katazo la Mifuko ya Plastiki na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ameahidi kusimamia utekelezaji wa katazo la kisheria la matumizi ya mifuko ya plastiki, usimamizi wa biashara ya kaboni ili kuongeza msukumo wa sekta hifadhi ya mazingira nchini.

Mhe. Mhandisi Masauni amesema hayo leo Desemba 13, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliyehamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri Masauni amesema mwaka 2019 Serikali ilitoa maelekezo mahsusi kuhusu katazo la mifuko ya plastiki na kusema Ofisi hiyo itaongeza kasi ya usimamizi wa katazo hilo ili kulinda afya ya jamii, Wanyama na mazingira.

“Tutashirikiana na Menejimenti ili kuhakikisha tunaongeza kasi katika kusimamia masuala ya katazo la mifuko ya plastiki, usimamizi wa biashara ya kaboni na utoaji wa vyeti vya tathimini ya mazingira (EIA) ili kufikia malengo tuliyojiwekea” amesema Waziri Masauni.

Kwa upande mwingine Waziri Masauni ameahidi kushirikiana na Menejimenti na watumishi wa ngazi zote ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo katika kuwahudumia wadau mbalimbali kupitia sekta za Muungano na Hifadhi ya Mazingira nchini.

Amesema milango ya Ofisi yake ipo wazi kwa ajili ya kutoa ushirikiano unaohitajika na kuahidi kufanya kazi kwa bidi, juhudi na maarifa pamoja na kuimarisha ushirikiano na menejimenti na watumishi ili kutimiza maono ya Viongozi Wakuu wa Serikali katika kutoa huduma bora na stahiki kwa wananchi.

Awali akikabidhi Ofisi hiyo kwa Mhe. Waziri Masauni, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano na utendaji kazi wenye tija katika kipindi alichohudumu katika ofisi hiyo.

“Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ina watumishi wenye weledi, ari na morali ya kazi. Nawashukuru kwa ushirikiano mlionipatia katika kipindi cha miezi mitano niliyofanya kazi katika ofisi hii” amesema Mhe. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji amemueleza Waziri Masauni kuwa suala la hifadhi ya mazingira ni miongoni mwa agenda muhimu katika majukwaa ya kimataifa kwa sasa ambayo Tanzania imeendelea kunufaika nayo na kutolea mfano biashara ya kaboni ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) imekuwa ikiratibu.

“Hadi sasa kuna makampuni 63 yaliyojisajili katika kituo cha NCMC. Biashara ya kaboni ni fursa ambayo bado hatujaweza kunufaika nayo vizuri, ni biashara yenye faida kubwa kupitia sekta ya hifadhi ya mazingira. Kunahitaji jicho la karibu ili jamii yetu iweze kunufaika” amesema Mhe. Kijaji

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja alimshukuru Waziri Kijaji kwa kuIsimamia vyema Menejimenti ya Ofisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake na hivyo kuleta manufaa na tija katika masuala ya Muungano na hifadhi ya mazingira.

“Mhe. Waziri Kijaji tunakushukuru kwa uongozi wako kwani katika kipindi tulichokuwa nawe tumeweza kupiga hatua kubwa na mfano mojawapo ni kupitia Kituo cha NCMC ambapo tumeweza kusajili makampuni 63 ya biashara ya kaboni na tumejipanga hadi kufikia mwezi machi, 2025 tuwe na makampuni 100” amesema Waziri Kijaji.

Itakumbukwa kuwa tarehe hivi karibuni Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ambapo alimteua Mhe. Mhandisi Hamad Masauni kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).




Related Posts