Yanayochangia kuharibu valvu za moyo kwa mtoto

Dar es Salaam. Kutotibiwa mapema magonjwa ya mafua yanayosababishwa na bakteria, nimonia na mafindofindo ‘tonsillitis’ imetajwa kuchangia uharibifu wa milango ya moyo, maarufu kama ‘valvu’.

Valvu ni sehemu za moyo zinazofanya kazi kama milango inayofunguka na kufunga, inayosaidia kuruhusu damu kutiririka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Valvu zinapochoka au kuharibiwa, mtu hupata ugonjwa wa moyo na hivyo inapaswa kufanyiwa marekebisho au kubadilishwa.

Valvu huhakikisha damu inaenda kwa wakati na kwa mwelekeo sahihi, zinapofunguka na kufunga, hutengeneza sauti ambazo ndiyo mapigo ya moyo.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkurugenzi wa upasuaji wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Angela Muhozya anataja miongoni mwa sababu za mtoto kupata changamoto ya valvu ni kutotibiwa mapema akipata maradhi ya mafua yatokanayo na bakteria.

Anasema safari ya mtoto mwenye shida ya valvu za moyo inaanzia pale anapougua mafua yanayosababishwa na bakteria hao ambayo mara nyingi, yanasababishwa na mazingira machafu au kuishi nyumba isiyo na hewa ya kutosha.

“Ni vigumu kutofautisha mafua ya bakteria na ya virusi, lakini yanayosababishwa na bakteria mtoto anakuwa na homa kali na nimonia,” anabainisha.

Kitaalamu, bakteria hao wamefanana na misuli iliyopo kwenye moyo, hivyo mwili unatengeneza kinga kupigana na bakteria hao ambapo kinga iliyotengenezwa inaenda kupigana pia na misuli hiyo ya moyo ikidhani ni bakteria kwa kuwa inafanana kisha kuharibu valvu.

“Kwa kuwa wazazi wengi hawatambui suala hili na kutokana na mazingira wanayoishi na watoto hao, ugonjwa unakuwa wa kujirudiarudia kwa mtoto, kinga nayo inakuwa inaharibu kidogo kidogo valvu za moyo.

“Hali hii inatokea pale mtoto asipotibiwa mafua hayo, lakini endapo akitibiwa mapema akapewa dawa mwili hautatengeneza kinga nyingi, hivyo madhara hayawezi kwenda kwenye moyo,” anabainisha.

Lengo la kinga ya mwili ni kuharibu bakteria na si moyo, lakini kwa kuwa ugonjwa unajirudia, kinga hiyo inaharibu pia milango ya moyo kidogokidogo ambapo kuanzia umri wa miezi sita hadi akifikisha miaka kuanzia 10 hadi 15 madhara yanaanza kujitokeza.

“Mlango umeundwa kwa nyama, kinga hiyo inapoharibu unatengeneza kidonda, baada ya kidonda kupona mlango unakakamaa na kuwa mdogo kupitisha damu kutoka kwenye moyo kwenda mwilini au kutoka mwilini kwenda kwenye moyo,” anasema.

“Kuna wakati bakteria anashambulia mlango unakuwa mkubwa sana, damu inakuwa inavuja. Kawaida ya mlango unafunga na kufungua ili damu ipite ipasavyo, sasa ukiliwa unatanuka na kuwa wazi,” anafafanua.

Anasema baada ya mchakato huo kuanzia mtu anapokuwa mdogo dalili zake zinaanza kuonekana akiwa na miaka kuanzia 10 hadi 15, ambapo moyo unakuwa umefikia hatua mbaya ya kuharibika.

Bila shaka umewahi kusikia kuhusu ugonjwa wa mafindofindo, kama yalivyo maradhi mengine huwashambulia watoto wadogo pia na yasipotibiwa ipasavyo, yanaweza kuwa chanzo cha maradhi ya moyo kwa kundi hilo.

Wanasema watoto wasiopatiwa kwa usahihi tiba ya ugonjwa huo na ukawa unawapata mara kwa mara, wanaweza kuwa katika hatari ya valvu zao za moyo zikashambuliwa na bakteria.

Daktari bingwa wa maradhi ya moyo kwa watoto kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Naiz Majani, anautaja kitaalamu ugonjwa wa mafindofindo kuwa ni ‘Pheumatic Heart Disease’, ndio unaosababisha kwa kiasi kikubwa tatizo la moyo kwa upande wa valvu.

Anasema mafindofindo husababishwa na mambo mawili ambayo ni virusi na bakteria. “Ikiwa yanasababishwa na virusi hayana shida, ila yakisababishwa na bakteria aitwaye kitaalamu Streptococcus ambaye husababisha maradhi hayo kwa asilimia tatu, hapo anakuwa kwenye hatari ya kupata tatizo la moyo kwenye valvu iwapo hatapatiwa matibabu ya kina.”

Dk Majani anasema bakteria huyo anaposhambulia huamsha walinzi wa mwili ambao huanza kuwashambulia wadudu hao. “Kibaya zaidi, bakteria huyo ana vitu vinavyofanana sana na vya mwili wa kwenye valvu za moyo, kwa hiyo, askari wa mwili wanapowashambulia bakteria hao, hushambulia na valvu wakidhani wanapambana na adui, hivyo kuleta hitilafu kwenye moyo.”

Akitaja dalili za kuharibika kwa valvu, Dk Muhozya anasema ni pamoja na kusikia maumivu ya kifua, kushindwa kufanya kazi, kushindwa kupumua, uchovu na hata udhaifu.

Dk Muhozya anasema wagonjwa wengi wanatoka katika maeneo ya Arusha, Kilimanjaro, Singida, Karatu na katika mazingira magumu wanayotoka watu yasiyo salama, ikiwemo kuwa na madirisha yasiyopitisha hewa ya kutosha.

“Hata hivyo, siku zinavyokwenda idadi inapungua kutokana na elimu ya afya inayotolewa na Serikali kupitia wataalamu wa JKCI,” anasema.

Changamoto kubadilishiwa valvu

“Zamani wagonjwa walikuwa wanakuja wakiwa na miaka 25 na valvu mpya tutakayomuwekea inakaa kwa miaka 15 hadi 20, hadi ikija kuchoka anakuwa na miaka 40 hadi 45 ambapo siyo umri wa kufanya kazi nzito zenye kuhitaji damu nyingi,” anasema.

Anasema kwa sasa mgonjwa akifika na miaka 10 akiwekewa valvu, akifika miaka 25 inakuwa imeshachoka inahitaji kubadilishiwa, changamoto ni kwamba upasuaji wa mara ya pili ni hatari kwa kuwa kuna uwezekano wa kupoteza damu nyingi,” anasema.

Changamoto nyingine ni masharti ya vyakula ambavyo havitakiwi ili kuepusha damu kuganda, masharti ambayo mtoto ni vigumu kuyatimiza kuliko mtu mzima.

Mtoto akiwekewa valvu uwezekano wa kunywa dawa kila siku maisha yake yote inakuwa changamoto.

Anasema valvu bandia zinatengenezwa kutoka kwa wanyama, ingawa mwili wa binadamu una tabia ya kukataa vitu ambavyo siyo vyake kwa kugandisha damu eneo husika. Hivyo katika valvu ya bandia damu inaweza kuganda ikaziba, ndiyo maana mgonjwa anapaswa kunywa dawa maisha yake yote ili kusaidia damu kutoganda.

Katika kupambana na changamoto hiyo, wataalamu wa upasuaji wa moyo wa JKCI, wamepewa mafunzo ya kutibu valvu za moyo kwa kuzirekebisha badala ya kuzitoa na kuweka za bandia.

Mafunzo hayo yametolewa na wataalamu wa afya kutoka Shirika la Open Heart International la nchini Australia kwa kipindi cha wiki moja.

Daktari kutoka Shirika la Open Heart International la nchini Australia, Dareen Wolfers anasema katika kambi hiyo wamekuja kwa ajili ya kuongeza ujuzi kwa wataalamu wote wanaomhudumia mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa moyo, hivyo kuleta wataalamu wa upasuaji, wataalamu wa usingizi, madaktari na wauguzi wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) cha wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo.

Ofisa Uuguzi wa JKCI aliyepata mafunzo kupitia kambi hiyo, Lilian Peter, anasema yatamsaidia kuweza kutambua kwa haraka changamoto anazopitia mgonjwa na kuweza kumsaidia.

“Kupitia mafunzo haya naweza kusimama mwenyewe, nikamhudumia mgonjwa na kutambua matatizo ambayo mgonjwa anayapata na kumsaidia kwa wakati,” anasema Lilian.

Hata hivyo, kwa sasa JKCI inatoa huduma hiyo inayowarahisishia Watanzania wanaosumbuliwa na maradhi hayo kwa bei nafuu ukilinganisha na kwenda nje ya nchi.

Related Posts