Minyukano baina ya timu Tundu Lissu na Freeman Mbowe juu ya nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema, imemuibua Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, safari hii akija na maswali manne.
Lissu ametangaza kuwania uenyekiti wa Chadema katika uchaguzi ujao, akitaka kumrithi Freeman Mbowe anayekiongoza chama hicho tangu mwaka 2004.
Hatua hiyo, imeibua minyukano ndani na nje ya Chadema hususan mitandaoni.
Askofu Bagonza katika andiko lake ameibua maswali manne na ushauri wa nini wafanye timu hizo mbili zinazonyukana.
Mosi, kama katumwa na CCM au anajiandaa kuhamia CCM/ACT, kwa nini mvuane nguo na kukipasua chama kwa mtu anayeondoka? Halafu akiondoka mnaanza kukiunganisha wakati mlikipasua wenyewe?
Pili, kama yeye ni imara, chama imara, wapiga kura wengi wako naye; kwa nini mhangaike na asiye na wapiga kura na mkipasue chama kwa mtu asiye na wapiga kura?
Tatu, kama mwamuzi ni wapiga kura wa mkutano mkuu, kwa nini kupiga kampeni mitandaoni ambapo hakuna wajumbe wa mkutano mkuu? Sisi mnaotusumbua kwa kampeini zenu hatuna kura.
Nne, kama mnaamini amekaa sana; hana uwezo wa siasa za wakati huu, amerambishwa asali, kwa nini kukibagaza chama mitandaoni na msisubiri kubagazana ukumbini ambako kuna kura?
Baada ya kuibua maswali hayo, Askofu ametoa ushauri ufuatao:
“Pande zote zinatumiwa bila kujitambua. Biblia inamtaja mtu fulani kuwa ni “mpumbavu” kwa kuwa anaivunja nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.
Laiti mngejua mnavyotukera! Azimeni hekima ya Mfalme Suleimani juu ya wanawake wawili waliogombania mtoto. Mtoto huyo ni CDM. Anayesema tugawane mtoto, huyo mtoto si wake. Anayesema chukua mtoto hata kama si wako bora aendelee kuishi, huyo ndiye mwenye mtoto”