Baa, hoteli Zanzibar zapewa siku sita za kupiga muziki mwisho wa mwaka

Unguja. Wakati wamiliki wa baa na hoteli waliofungiwa kupiga muziki wakiomba waruhusiwe kufanya hivyo kwa Desemba, Serikali imewapa ruhusa ya kufanya hivyo kwa  siku sita pekee.

Oktoba 18, 2024, Serikali kupitia Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni ilitangaza marufuku ya kupiga muziki kwenye baa na hoteli zote zisizo na mifumo ya kudhibiti sauti ili isivuke mipaka ya maeneo yao.

Hata hivyo, wamiliki wa baa na hoteli wameomba kupunguziwa ukali wa agizo hilo kwa kipindi cha mwisho wa mwaka, wakisisitiza kuwa Desemba ni mwezi muhimu wa biashara kutokana na msimu wa sikukuu.

Hata hivyo, katika mkutano uliofanyika leo, Desemba 14, 2024, mkoani Kusini Unguja kati ya wafanyabiashara hao na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alitangaza kuwa Serikali itaruhusu muziki kupigwa kwa siku sita pekee.

“Siku nne kuanzia Desemba 24 hadi 27, 2024 na siku mbili za mwanzo wa mwaka mpya 2025. Lakini nawasisitiza kuwa kiwango cha sauti kisizidi kiwango cha ‘volume 40’,” amesema waziri huyo.

Hata hivyo, wamiliki hao wamesema kuna baadhi ya hoteli na baa ziko mbali na makazi ya watu, hivyo walimweleza waziri kuwa agizo lililotolewa nalo halikulizingatia hilo, linapaswa kupitiwa upya.

Akitoa maoni katika mkutano huo, Meneja wa Sunner Jungle Club, Kassim Mohd amesema biashara zao zinaimarika zaidi katika mwezi huu hivyo wanaomba waruhusiwe wapige muziki kwa mwezi huu mpaka uishe.

“Zuio hilo limekuja wakati wa biashara, mwezi huu ndio wageni wengi wanakuja kusherehekea sikukuu ya Krismas kisiwani hapa. Tunaomba tuachiwe kwa kipindi hiki,” amesema Kassim. 

Naye Mwakilembe Daniel amesema wananchi ambao wanalalamika kuwa wanapigiwa kelele ndio ambao wamejenga baada ya sehemu hizo kufanyiwa uwekezaji wa kumbi za starehe.

“Wananchi wanaolalamika kuwa wanapigiwa kelele ndio wao ambao wamezifuata hizi kelele kwa sababu baadhi ya maeneo tayari yalishajengwa kabla ya kuhamia wao,” amesema Mwakilembe.

Mmiliki wa Hoteli ya Avrora Boutique iliyopo Jambiani, Marisa Baretta amesema baadhi ya wamiliki wa baa wanaopiga muziki katika maeneo yao, wanakera wageni kwa sababu wengi hawapendelei kelele.

Amesema Serikali inapaswa kuliangalia vyema jambo hilo na wasilikalie kimya kwa sababu baadhi yao wanakosa oda za wageni kutokana na kelele za muziki kutoka kwa baadhi ya majirani zao.

“Baadhi ya wageni wanashindwa kukaa katika hoteli zetu na hawapendelei kelele, wengine wanalala ila hawataki kulipa wanadai hawakupata kupumzika, jambo hilo linakuwa hasara kwao,” amesema Marisa.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri Tabia amesema: “Tunawapa ofa ya kupiga muziki kwa siku sita kati ya hizo, nne Desemba na mbili za mwaka mpya ila mnapaswa kupiga kwa kiwango cha sauti kisichozidi volume 40.”

Amesema ataichukua michango na changamoto zilizotolewa hapo na ataziwalisha katika ngazi za juu, kwa lengo la kutafuta njia ya kuwapa ahueni wadau hao.

Related Posts