Equity Bank na ADC Tanzania Yaanzisha Programu ya Mafunzo kwa Wafanyabiashara Wanawake

Programu hii inalenga kuwasaidia wanawake kuongeza uwezo wao wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na kuwa na vigezo vya kupata mikopo kupitia dawati la Mwanamke Plus lililoanzishwa kwa ajili ya biashara za wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Desemba 13, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ADC Tanzania, Esther Kitoka amesema wamekuja na programu hiyo baada ya kufanya tathimini kwaa Afrika nzima na kuona kuna upungufu mkubwa wa mabenki kutoa mikopo kwa Wajasiriamali wadogo na wa kati hasa wanawake.

“Tunachoangalia zaidi ni kuhakikisha kwamba zile biashara zinakua, zinakuwa endelevu ili ziweze kurithishwa kwa vizazi na vizazi”. Amesema

Aidha amesema wameona waingie katika eneo hilo wakishirikiana na wadau hao ili waweze kuhakikisha wanawasaidia wanawake waweze kukuza biashara zao na waweze kupata mikopo.

“Tutawafundisha kwa siku moja , baada ya hapo tutaenda kwa mmoja mmoja kwasababu changamoto zinapishana, wengine wanachangamoto za masoko, wengine changamoto ya uongozi, wengine katika kuweka mahesabu”. Amesema

Amesema katika programu hiyo ya mwaka mmoja wanatarajia kuwafikia wanawake zaidi ya 100  katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar na kuweza kupata mikopo.

Kwa upande wake Meneja wa Mafunzo kutoka Bank ya Equity Tanzania, Martine Rajab amesema kutokana na uhaba wa elimu ya fedha na biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, wameamua kuanzisha darasa la mafunzo ya vitendo kwa watu 100 ambao wataanza nao kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Tutapita kwa mfanyabiashara mmoja baada ya mwingine, tukiendelea kumfundisha, ni kozi ya mwaka mzima, ambao lengo letu mtu huyu aweze kukopesheka na kumfundisha namna ya kupata masoko ndani na nje ya nchi”. Amesema

Kwa upande wake Mshiriki wa Mafunzo hayo Mjasiriamali, Cotrida Kagaruki amesema kupitia mafunzo hayo yatakwenda kuwasaidia namna ya kusimamia na kuratibu biashara zao.

Amesema wamefundishwa kuhusu utawala wa fedha, namna ya kusimamia mradi, kuwa na mipango mkakati na matumzi mazuri ya fedha ambazo watakuwa wanazipata.

Pamoja na hayo amesema wamekuwa wakihudhuria semina mbalimbali lakini semina hiyo ni ya tofauti kwasababu watakuwa wanakuja kwenye biashara zao na kuangalia ni wapi wanafanya vizuri na ni wapi wanakosea.

Related Posts