Kauli ya Serikali sakata la kuzuiwa Air Tanzania Ulaya

Dar es Salaam. Wakati  taarifa ya ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuzuiwa kuingia katika anga la nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zikisambaa, Serikali imefafanua ikisema ipo kwenye mazungumzo.

Taarifa iliyotolewa na EU, ilionyesha ndege za Air Tanzania zimeongezwa katika orodha ya ndege zilizofungiwa kuingia katika nchi zake 27, japokuwa bado shirika hilo halijaanza safari za kwenda nchi hizo.

Akilizungumzia suala hilo jana Ijumaa Desemba 13, 2024 Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema shirika hilo lipo kwenye majadiliano na mamlaka za Ulaya kwa ajili ya kuyafikia masharti husika.

“Shirika letu la ndege halijaanza safari za Ulaya, isipokuwa lipo katika mchakato wa kuanza safari za Ulaya, na katika kufikia hatua hiyo, yapo masharti yanatakiwa yatimizwe ya eneo hilo ambayo kila ukanda wanakuwa nayo.

“Kwa hiyo shirika lipo kwenye mchakato kwa kushirikiana na mamlaka za Ulaya kupata kibali cha kuruka ama kutua katika anga la Ulaya, Sasa hiyo isiwe tafsiri ya kuzuiwa. Ni kwamba tupo kwenye mchakato wa hatua kwa hatua,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa tayari wataalamu wa masuala ya anga kutoka EU wamefika nchini na wapo katika mazungumzo ATCL kuona namna ya kupata vibali hivyo.

Awali, taarifa ya EU iliyosambaa, ilitaka miongoni mwa vigezo vya kuzifungia ndege za Air Tanzania ni kutokukidhi kwa vigezo vya  usalama wa anga vya kimataifa.

“Umoja wa Ulaya leo umerekebisha orodha yake ya mashirika ya ndege  yanayozuiwa kuingia, au kuwekewa vikwazo vya kiutendaji katika kuingia  Umoja wa Ulaya. Kutokana na taarifa hii, Air Tanzania imeongezwa kwenye orodha hiyo,”imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, Air Tanzania inatambulika na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) tangu ilipoanzishwa mwaka 1977, ambapo miongoni mwa vigezo vya kuwa mwanachama wake, ni kufuata viwango vya kimataifa vya usalama wa anga na utendaji.

Ndege nyingine zilizoingizwa katika katazo hilo ni pamoja na:  Air Zimbabwe  (Zimbabwe) Avior Airlines (Venezuela), Blue Wing Airlines (Suriname), Iran Aseman Airlines (Iran), Fly Baghdad (Iraq) and Iraqi Airways (Iraq).

Akizungumzia orodha hiyo, Kamishna wa Usafiri na Utalii wa Umoja wa Ulaya, Apostolos Tzitzikostas, amesema lengo ni kuhakikisha mashirika hayo ikiwemo Air Tanzania yanaongeza sifa na vigezo.

“Uamuzi wa kuijumuisha Air Tanzania katika orodha, ni kwa sababu ya dhamira yetu thabiti ya kuhakikisha kuwa kuna  viwango vya juu zaidi vya usalama kwa abiria barani Ulaya na duniani, “amesema na kuongeza:

“Tunaihimiza  Air Tanzania kuchukua hatua za haraka na thabiti kushughulikia masuala haya ya usalama wa anga. Kamisheni yetu itakuwa tayari kutoa msaada kwa  mamlaka za Tanzania katika kuboresha usalama wa ndege za Air Tanzania na kuwezesha kufikia vigezo vyote vya usalama wa ndege kimataifa.

Related Posts