Mirerani. Madini tofauti yenye uzito wa gramu 184.06 na thamani ya Sh3.1 bilioni yanatarajiwa kuuzwa na kununuliwa kwenye mnada wa madini ya vito unaofanyika mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 14, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, wakati wa uzinduzi wa mnada huo ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Mbibo amesema mnada huo unahusisha wafanyabishara 195 wakiwemo wanunuzi wakubwa 59, wadogo 120, wachimbaji madini tisa na waongeza thamani saba.
“Tanzania ina madini mbalimbali ya vito ikiwemo Tanzanite, Spinal, Ruby, Garnet na mengineyo na tumerejesha minada hii kwa lengo la kuongeza thamani madini yetu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema mnada huo utaongeza thamani na uchumi kwa wakazi wa eneo la mji mdogo wa Mirerani.
Sendiga amesema ujenzi wa soko la madini unaondelea mji mdogo wa Mirerani, ukikamilika utaongeza tija kwa wafanyabishara wakubwa na wadogo.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia mkoa wa Manyara fedha za maendeleo zaidi ya Sh600 bilioni ambazo nyingine zipo sekta ya madini na tunatarajia soko la madini likikamilika litawanufaisha wana Manyara,” amesema.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amepongeza Waziri Mavunde kufanikisha mnada huo kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Hata hivyo, Ole Sendeka amekemea vikali ucheleweshaji wa upekuzi kwa watu wanaotoka ndani ya ukuta, kwani vyumba vichache ndiyo vilitumika kwa kisingizio cha ukarabati wa vyumba vingine, hivyo kutumia muda mrefu.
“Watu wamelalamikia muda mrefu unaotumika kukaguliwa hivyo kuwa kero na nilimpigia simu mkuu wa wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala, ili angaalie suala hilo kwani limekuwa kero,” amesema Ole Sendeka.
Mkurugenzi wa kampuni ya Lucid Dream LTD, Upendo Kibona amesema anatarajia mnada huo kuwa na tija zaidi kwani utahusisha wauzaji na wanunuzi mbalimbali.
Kibona amesema Serikali inapaswa iongeze kufanyika minada ya kimataifa mara kwa mara, ili kuongeza thamani hayo kwani ilisimama kwa muda mrefu.
Amesema mnada huo ni mzuri kwa wafanyabishara na Serikali japokuwa mfumo wa Serikali nao ni mpya wa kujiandikisha kwenye mtandao.
Dalali wa madini ya Tanzanite, Sweet Nkya amesema mnada huo wa madini ya vito unatarajiwa kuuchangamsha kiuchumi mji mdogo wa Mirerani.
“Japokuwa mnada umehusisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo, ni changamoto tu lakini tunatarajia kunufaika kupitia tukio hilo la leo Desemba 14, 2024,” amesema Nkya.