Maelfu kufurika kwenye mkesha wa Mwamposa kwatazamwa kwa sura mbili

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine, maelefu ya wakazi jijini hapa na wengine kutoka mikoa na nchi mbalimbali wamefurika katika mkesha uliopewa jina la ‘Kuvuka (mwaka) kabla ya Kuvuka wa kanisa la Inuka Uangaze linaloongozwa na Mtume Boniface Mwamposa, unaotazamwa na wachambuzi wa masuala ya kijamii sura mbili tofauti.

Mkesha huo uliofanyika Desemba 13 hadi 14, 2024 katika uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.

Mkesha huo ni miongoni mikusanyiko mikubwa iliyowahi kufanywa na Mtume Mwamnposa maarufu Bulldozer, ukiwemo wa Desemba 18, 2022, ambapo wafuasi wake waliujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na wengine kubaki nje.

Februari mosi 2020 watu 20 walifariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa katika Uwanja wa Majengo mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro walipokuwa wakikanyaga mafuta ya upakoyaji liyomwagwa kwenye milango ya kutokea uwanjani, wakati Mwamposa akiendesha ibada.

Mtume Boniface Mwamposa wa kanisa la Inuka Uangaze akiwaongoza maelfu ya wananchi katika mkesha uliofanyika uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.

Wingi wa watu katika kusanyiko hilo, umesababisha foleni kubwa ya magari Ijumaa jioni na Jumamosi asubuhi, ugumu wa usafiri kwa waliohudhuria na neema ya kipato kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Mkusanyiko huo na mingine ya aina hiyo inaelezwa na mwanasaikolojia Jacob Kilimba kuwa inajaza watu kutokana na hali ngumu wanazopitia watu katika nyanja mbalimbali.

“Kiuhalisia watu wanapitia mambo mengi magumu na hawana pa kuyapeleka. Bahati mbaya zaidi kuna ombwe la utatuzi wa matatizo ya watu, mtu akibaki nyumbani ataishia kuambiwa pole au avumilie.

“Ndio maana watu wanakwenda kwenye maombezi ambako wakifika wanaomba na kuimba kwa sauti kubwa na kwa kufanya hivyo wanapata ahueni ya maisha wakiamini Mungu atawajibu,” amesema.

Mbali na mtazamo huo, mwanasaikolojia Saldin Kimangale anaiona mikusanyiko hiyo na dhana ya kufuata mkumbo.

“Hii inatawaliwa na dhana ya “Mob Psychology” kwa maana ya kufuata mkumbo. Watu wengi hujiunga kwenye msafara ili wakashuhudie msafara ulivyo mrefu au umati ulivyo mkubwa.

“Watakwenda viwanjani ili wakaone namna watu walivyojaa kumbe nao wanaongeza idadi, na wengi wao wanakwenda hawana malengo yoyote zaidi ya kusema “kulikuwa na watu wengi si mchezo”

Hata hivyo, sawa na Kilimba,  Kimangale amesema pia watu wanatafuta faraja, wakiamini Mungu huleta faraja kwa watu.

“Kisaikolojia tunaichukulia kama ni kinga,”  amesema.

Amehusisha pia imani za maombezi na matatizo ya afya ya akili yakiwamo ya mtu kuwa na imani kubwa sana kuhusu jambo fulani la kidini, hata kama jambo hilo sio kweli.

 “Ziko tabia za kupagawa au kupandwa na midadi (mimicking) ambapo unapomuona mtu anafanya jambo fulani na wewe unapata mijongeo au misukumo kama hiyo na unashindwa kujizuia, hili nalo hudhihirika sana kwenye mikusanyiko ya kidini, na mbaya zaidi wanapojeruhiwa au kufia huko huamini kuwa ni baraka,” amesema.

Maelefu ya wananchi wakiwa wamefurika katika mkesha ulioandaliwa na Mtume Boniface Mwamposa wa kanisa la Inuka Uangaze katika uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe.

Dalili za wingi wa watu katika mkesha huo zilianza kuonekana Ijumaa mchana, magari hali ya usafiri wa kuelekea Kawe ilikuwa ngumu na daladala zinazoelekea eneo hilo zilipandisha nauli na kutoka Sh600 hadi Sh2, 000, huku pia foleni ikitawala kuelekea eneo la Tanganyika Packers.

Watu mbalimbali walianza kuwahi nafasi kuanzia Ijumaa saa 12 asubuhi, hususani wale ambao walikuwa wametoka mikoa na mbalimbali na hadi usiku wa manani uwanjwa ulikuwa umefurika.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni kutoka Ujerumani, Italia, Ubeligiji, ambao Mtume Mwamposa aliwapa nafasi kwenda mbele wakipeperusha bendera za mataifa yao.

Wageni wengine walitoka Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Congo, Uganda na Kenya, huku wengine wakishiriki mitandaoni na kwenye televisheni zilizokuwa zinarusha matangazo mubashara.

Ibada ya mkesha ilianza saa 12 jioni, ambapo nyimbo za sifa ziliimbwa na wasanii wa muziki wa injili na kukiwa na vipindi vya kutoa shuhuda na sadaka.

Mtume Mwamposa alifika uwanjani hapo saa 6:09 usiku akipokewa na wasaidizi wake huku ulinzi ukiwa umeimairisha na askari polisi na Suma JKT.

Baadaye viongozi mbalimbali waliwasili akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule.

Azungumza katika mkesha huo, Chalamila alieleza namna alivyofanyiwa maombi na Mwamposa akiwa mkoani Mbeya na muda mfupi baadaye ateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Chalamila aliwananga baadhi ya watu wanaosema shuhuda za nabii huyo ni za kutengeneza, akisisitiza wana wivu.

“Nikiwa Mbeya usiku kwenye send-off nilisalimiana na Mwamposa na akanishika mkono akaniambia tuonane kwa ajili ya maombezi,” alisema.

Amesema Mwamposa alimwambia kiti chake hakijachukuliwa na wataendelea kuomba zaidi ili mamlaka ziendelee kutenda haki, kumfahamu na kuongoza watu kwa furaha na upendo.

“Baada ya maombezi wakati narudi kabla ya kufika hoteli niliyofikia, nikaangalia simu na kuona nimeteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera,” amesema.

Chalamila amesema wakati Mwamposa akiomba kibali cha mkesha huo, aligundua wapo watu wenye wivu wanapenyeza maneno yenye lengo la kuuzuia.

“Wakaleta maneno mengi kwamba mara hakuna usalama, mara sijui kitu gani, nikasema kwa sababu ni mkesha wa kumuita Mungu, Mungu mwenyewe atafanya njia katika mkesha huu, mbona watu wanakesha baa wakinywa bia?” amehoji.

Amesema taarifa za vikwazo vya mkesha huo zilimfikia Rais Samia Suluhu Hassan, lakini akaruhusu na akamwagiza Chalamila apeleke sadaka yake kwenye mkesha huo.

“Rais Samia Suluhu Hassan amenituma nimwambie Mwamposa kwamba aendelee kuhubiri kwa sababu anamsaidia sana.

“Kwa hiyo tunaposema muombeeni Rais, anaweza kuingia rais ambaye hamjui Mungu na halitaji jina la Mungu na akaamuru makanisa yavunjwe. Tujue tumetenda dhambi ya kutomwombea Rais anayemtaja Mungu kama zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe, ili Taifa letu lisonge mbele,” amesema.

Kuhusu suala la usalama, Chalamila amesema tangu aingie ndani ya mkoa wa Dar es Salaam kundi la panyarodi halijaonekana wala watu wanaochinja wenzao.

Awali, kabla ya kumkaribisha Chalamila, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila amekumbusha jinsi Mwamposa alipotembelea mkoani Kagera wakati yeye akiwa katibu tawala wa mkoa huo.

“Ulikuja nikiwa katibu tawala Kagera na ndugu yangu Albert Chalamila alikuwa mkuu wa mkoa, ulinena maneno ya kwamba ungetamani tuwe karibu muda wote, ungetamani huduma tuliyokuwa tukifanya Kagera mimi na Chalamila tungekuwa pamoja.

“Nakumbuka Chalamila alitangulia Dar es Salaam amehudumu kwa miezi saba, lakini baada ya miezi saba na mimi nikatoka Kagera niko Dar es Salaam,” amesema.

Akihubiri katika mkesha huo, Nabii Mwamposa amesema hakujua siku mkuu wa mkoa aliyopeleka sadaka kanisani, alimpigia simu na kumweleza kuwa yupo kanisani kwake na kuwa hakuwa anafahamu chochote juu ya ujumbe alionao.

“Nilimkaribisha na yeye ni mnyenyekevu, nikamwambia karibu ibadani, baadaye nilimpa asalimie anakuja na sadaka, kumbe Rais Samia Suluhu Hassan amemwambia aniletee sadaka.

“Ungeikataa sadaka? Kuna watu wakasema ifungue. Nifungue ya nini imeletwa madhabahuni, sadaka inafunguliwa na makuhani, wengine wakifungua macho yataharibika,” amesema.

Sababu, manufaa ya kufurika

Baadhi ya watu waliohudhuria mkesha huo wameeleza kuwa mkesha umekidhi matarajio yao.

Mkazi wa Morogoro Shihuda Luhumbika amesema amewaleta wagonjwa wawili wanaosumbuliwa na miguu na moyo kwa muda ambao waliposikia kuhusu mkesha, waliwahi ili kupata uponyaji.

“Nikiachana na hao wagonjwa, kilichonipa moyo ni baada ya kuambiwa kushika ninachotaka kupata mafanikio, kwa sababau mimi ni mkulima nimechukua udongo kutoka shambani kwangu na ninaamini mwakani nitavuna pakubwa,” amesema Shihuda.

Gaudensia Sambala, mkazi wa Njombe amesema amekuja kwa ajili ya upatanisho na ndugu zake baada ya kufarakana kwa muda mrefu wakigombania mali.

“Nimekuja na nguo ambazo nitawapa ndugu zangu baada ya kufanyiwa maombi ya uhakika na ninaamini Mungu anakwenda kuonyesha miujiza yake na kumaliza tofauti zetu,” amesema.

Baada ya mkesha huo ulioisha leo Jumamosi saa 2 asubuhi, maelfu ya waumini wamekwama kupata usafiri kutokana na uhaba wa mabasi yaliyokuwa yakifika eneo hilo na wiki wa watu.

Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwepo eneo hilo ameshuhudia baadhi ya mabasi yasiyokuwa ya njia za Kawe yakisaidia kupunguza adha hiyo, huku wengine wakitembea kwa miguu kutoka Tanganyika Packers hadi Lugalo kupata unafuu wa usafiri.

Waumini hao wakiwamo wanawake wenye watoto wadogo, walionekana wamekaa karibu na barabara bila kujali usalama wao, huku pikipiki na bajaji zikisaidia kuwasomba baadhi yao.

Wananchi waliohuduria mkesha katika uwanja wa Tanganyika Packers Kawe wakiwa kituoni wakisubiri usafiri wa kurudi nyumbani kwao baada ya kumalizika kwa mkesha.

“Nasubiri watu wapungue ndiyo niondoke, maana kila nikipiga hesabu ya nauli naona inanibana, hivyo ni vigumu kwangu kwa sababu kutoka hapa hadi Mbezi nauli Sh2, 000,” amesema Janeth Kimaro.

Amesema ni mara yake ya kwanza kufika katika mkesha huo na hakujua kama kunakuwa na changamoto ya usafiri, hivyo hakubeba fedha za ziada.

Naye Frank Mwaibungu amesema kinachomchanganya ni kuwa na watoto ambao wanahitaji kula na wameshaanza kulia njaa kwa sababu muda umekwenda wa kunywa chai Jumamosi asubuhi.

“Nina watoto watatu hawa hapa na wameanza kusumbua njaa usafiri unasumbua na siwezi kukodi bajaji hadi nyumbani Kitunda. Ninachofanya ni kuwapa juisi ili wapooze njaa,” amesema Mwaibungu.

Kulwa Isack (60), mkazi wa Mlandizi, Pwani  ameiomba Serikali iruhusu magari mengine kufika katika eneo hili ili kupunguza watu kutokana na shida ya usafiri iliyopo.

“Mgogoro wa kiwanja ndiyo umenileta huku kwenye mkesha. Nimekutana na shida ya usafiri sikujua hili, ningewahi mapema nilikuja na majirani zangu tumepoteana sijui sasa kama wameondoka au la,” amesema Kulwa.

Hata hivyo, kwa waumini waliotokea mikoa ya Njombe, Morogoro na Mwanza walibahatika kupata mabasi yaliyowafuata eneo hilo.

“Tunashukuru wameleta gari mpaka hapa lakini nauli imekuwa juu, kutoka hapa hadi Njombe nimeambiwa Sh55,000 wakati kutoka Mbinga hadi Dar es Salaam nilikuja kwa Sh46,000,” amesema Samwel Nyoni.

Wananchi waliohuduria mkesha katika uwanja wa Tanganyika Packers Kawe wakiwa kituoni wakisubiri usafiri wa kurudi nyumbani kwao baada ya kumalizika kwa mkesha.

Hata hivyo, mkatisha tiketi kwenye mabasi hayo, Christina Michael amesema: “Tunajua waliofika hapa wamekuja kwa sababu ya changamoto zinazowakabili na hatuwezi kusema tukate kwa bei ya chini kabisa, maana wakienda Mbezi nauli yake ni hizi hizi,” amesema Christina.

Baadhi ya wajasiriamali waliozungumza na Mwananchi katika eneo hilo, wamesema mkesha huo umeacha neema ya biashara kutokana na mauzo waliyofanya.

Debora Rashid, ambaye ni mamalishe, amesema kwa siku za kawaida huwa anauza kilo 20 za wali, lakini jana katika mkesha huo aliiuza kilo 80.

“Yaani jana tulipika tukapika tena, maana sufuria langu moja linapika kilo 20, lakini kutokana na umati wa watu uliokuwepo hapa nilijikuta napika sufuria nne,” amesema Debora.

James Leonard anayeuza vinywaji baridi, amesema huwa anauza katoni tano hadi 10, lakini kwa siku mbili hizi, amemaliza katoni 50.

“Japo watu wanakuja hapa kwa matatizo, lakini unatamani mikutano kama hii iwe walau kila mwezi ili nasi tufanye biashara, walau sasa nina uhakika watoto wangu hapa watapata madaftari na mabegi ya shule,” amesema James.

Naye Happines Masangu aneyeuza chips na mihogo, amesema kwa siku anauza Sh50,00 hadi Sh70,000 lakini katika mkutano huo ameuza Sh150,000, mauzo ambayo hayajawahi kufikia tangu aanze kufanya biashara eneo hilo miaka minne iliyopita.

“Asiyeshukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa hawezi kushukuru, niseme tu huu mkutano wengine umetunufaisha,” amesema Happiness.

Related Posts