Kilombero. Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Damas Ndumbaro amewahakikishia wafungwa katika magereza mbalimbali nchini, kuwa jopo la mawakili kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), litawafikia na kushughulikia changamoto zao za kisheria hususan rufaa.
Akizungumza na askari pamoja na wafungwa katika Gereza la Kiberege, wilayani Kilombero, Dk Ndumbaro amesema kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid, Serikali tayari imekubaliana na TLS kushughulikia matatizo ya kisheria waliyonayo wafungwa.
“Watakuja, wataandaa rufaa zenu na kuziwasilisha mahakamani. Rais Samia ameagiza kila mfungwa apate haki yake, kama kuna aliyeonewa basi upate haki yako,” amesema Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro amewakumbusha wafungwa kuwa gerezani ni sehemu ya adhabu, hivyo hawapaswi kuchagua magereza ya kwenda.
“Mfungwa hachagui gereza popote unapopelekwa, ni lazima ukubali kwa sababu Tanzania ni moja, na kila mwananchi ana haki ya kuishi popote,” amesisitiza.
Aidha, amesema msamaha wa Rais hutolewa kwa kuzingatia mwenendo mzuri wa mfungwa akiwa gerezani, hata hivyo, ameonya kuhusu makosa makubwa ambayo hayana msamaha, kama vile uhaini, mauaji, ubakaji, makosa ya kujamiiana na uhujumu uchumi.
Kuhusu kucheleweshwa kwa mahabusu kufikishwa mahakamani, Dk Ndumbaro amesema Serikali inaweka vifaa vya teknolojia vitakavyowezesha kesi kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
“Mahakama sasa zimeingia katika mfumo wa kimtandao, hii itawasaidia wafungwa na mawakili wao kusikiliza kesi wakiwa magerezani badala ya kusafirishwa kwenda mahakamani,” amefafanua Ndumbaro.
Wafungwa katika gereza hilo wametoa malalamiko kuhusu changamoto ya kukosa msaada wa kisheria, hali inayowakwamisha kutekeleza rufaa na kupoteza haki zao.
Pia wamemuomba Rais Samia kuongeza idadi ya wanaopewa msamaha kwani kwa sasa ni wachache wanaopata fursa hiyo.
Aidha, baadhi ya mahabusu wamelalamikia kucheleweshwa kwa kesi zao mahakamani, huku wakidai baadhi ya askari wamekuwa na tabia ya kuwapiga na kuwalazimisha kukubali makosa ambayo si yao.