Dar es Salaam. Maelfu ya wananchi waliohuduria mkesha wa Kanisa la Arise and Shine linaloongozwa na Nabii Boniface Mwamposa, wamekwama kupata usafiri baada ya kumalizika kwa mkesha huo katika uwanja wa Tanganyika Packers Kawe jijini hapa.
Mkesha huo ulioanza majira ya saa moja jioni ukihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam, mikoni na nje ya nchi, ukiwa na kauli mbiu ya Chako ni chako, umefungwa saa 2 asubuhi leo Desemba 14, 2014.
Waumini hao wamekwama kutokana na uhaba wa usafiri, hivyo wamejikuta wakirandaranda mitaani na wengine wakilala karibu na maduka na kwenye gereji za magari na bajaji.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwepo eneo hilo ameshuhudia baadhi ya magari yasiyokuwa na njia za Kawe yakisaidia kupunguza adha hiyo, huku wengine wakitembea kwa miguu kutoka Tanganyika Packers hadi Lugalo kupata unafuu wa usafiri.
Waumini hao wakiwamo wanawake wenye watoto wadogo wameonekana wakikaa karibu na barabara bila kujali usalama wao, huku pikipiki na bajaji zikisaidia kuwasomba baadhi yao.
Bila kujali usalama wao wapo waliokaa barabarani kabisa huku daladala, bajaj na pikipiki zikipita jirani na maeneo waliokaa jambo linalohatarisha usalama wao na watoto.
“Nasubiri watu wapungue ndiyo niondoke maana kila nikipiga hesabu ya nauli naona inanibana, hivyo ni ngumu kwangu kwa sababu kutoka hapa hadi Mbezi nauli Sh2,000,” amesema Janeth Kimaro.
Amesema ni mara yake ya kwanza kufika katika mkesha huo na hakujua kama kunakuwa na changamoto ya usafiri hivyo hakubeba pesa ya ziada.
Naye, Frank Mwaibungu amesema kinachomchanganya ni kuwa na watoto ambao wanahitaji kula, kwani wameshaanza kulia njaa kwa sababu muda umekwenda wa kunywa chai.
“Nina watoto watatu hawa hapa na wameanza kusumbua njaa usafiri unasumbua na siwezi kukodi bajaji hadi nyumbani Kitunda. Ninachofanya ni kuwapa juisi ili wapooze njaa,”amesema Mwaibungu.
Kulwa Isack (60), mkazi wa Mlandizi ameiomba Serikali kuruhusu magari mengine kufika katika eneo hili ili kupunguza watu kutokana na shida ya usafiri iliyopo na abiria kusimama mlangoni.
“Mgogoro wa kiwanja ndiyo umenileta huku kwenye mkesha, nimekutana na shida ya usafiri sikujua hili ningewahi mapema nilikuja na majirani zangu tumepoteana sijui sasa kama wameondoka au la, Naomba Serikali itusaidie kuruhusu magari kuja huku kupunguza hii shida,” amesema Kulwa.