Mwili wa mwanafunzi wa Rucu aliyeuawa wazikwa Ileje, baba ataka uchunguzi

Ileje. Wakati mwili wa Rachel Mkumbwa ukizikwa leo katika Kjiji cha Isongole kilichopo Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, baba mzazi wa binti huyo, Dickson Mkumbwa ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.

Rachel aliyekuwa akisoma mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) mkoani Iringa, alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake Desemba 12, 2024 kwa madai ya kubakwa hadi kuuawa.

Akizungumza baada ya binti yake kuzikwa, Mkumbwa amesema licha mwanawe kuzikwa, ameiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuwabaini na kuwakamata wahusika wote ili sheria ifuate mkondo wake na kukomesha vitendo hivyo.

Amesema unyama aliofanyiwa hauvumiliki kwani alikuwa akiishi kwa kumtumikia Mungu, lakini amefariki katika mazingira ambayo hayastahimiliki katika jamii.

Aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Rucu mkoani Iringa, Rachel Mkubwa enzi za uhai wake. Picha na Mtandao

Mkumbwa amesema kama familia wanalitegemea Jeshi la Polisi na Serikali kukamilisha upelelezi,  ambao utasaidia kuwakamata waliohusika kwani familia yake imeumizwa na taarifa za kifo cha mtoto wao.

Amebainisha kuwa anajua kifo kipo, lakini si kwa namna kifo cha mwanaye kilivyotokea, amesema katika kipindi hiki wanashindwa kuzungumza mengi zaidi kwa sababu wameumizwa mioyo yao.

“Nilisafiri kutoka Ileje mpaka Iringa baada ya taarifa ya kifo cha mtoto wangu, kwa kweli inaumiza, ndoto za mwanangu zimeishia hapa. Siwezi kuzungumza chochote, naishia hapa, tumwachie Mungu,” amesema baba huyo wa marehemu.

Kwa upande wake, mmoja wa wanafamilia, Hamisi Mkumbwa amesema kifo cha mdogo wao, kiliwashitua kwani walikuwa wanasikia kwa wengine mauaji ya aina hiyo, akisisitiza kwamba Jeshi la Polisi lihakikishe linawakamata wahusika wote.


DAKIKA ZA MWISHO KABLA YA KUBAKWA, KUUAWA MAJIRANI WASIMULIA TUKIO ZIMA MWANAFUNZI WA RUCU

Katika mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 13, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, marehemu alibakwa kisha watuhumiwa kuchukua simu yake ya mkononi.

“Tukio hili lilitokea Desemba 12 saa 5 usiku ambapo upelelezi umebaini watuhumiwa waliingia kwa jirani ambaye naye ni mwanafunzi na kuchukua simu mbili na kompyuta mpakato,” alisema kamanda huyo.

Marehemu Rachel alizaliwa Februari 17, 2005 katika Kijiji cha Malangali wilayani Ileje, alisoma shule ya msingi Ilulu kuanzia mwaka 2010 mpaka 2016, shule ya sekondari Consolata, kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 na elimu ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Ileje, kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.

Hadi umauti unamkuta Desemba 12, 2024, alikuwa akisoma katika Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), kitivo cha teknolojia ya habari na mawasiliano, akichukua Shahada ya Sayansi ya Elimu katika Teknolojia ya Habari  na Hesabu.

Related Posts