Dar es Salaam. Bodi ya Wataalamu ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imesema watahiniwa 663 kati ya 1,314 wa fani ya ununuzi na ugavi, wamefeli na watatakiwa kurudia baadhi ya masomo.
Pia bodi hiyo imesema watahiniwa 41 waliofeli kabisa watapaswa kuanza masomo yao upya.
Mbali na matokeo hayo, PSTB imetangaza kwa mara ya kwanza kuzalisha wakaguzi kwenye eneo la ununuzi na ugavi, ikitoa wito kwa waajiri kufadhili watumishi wao kwenda kupata mafunzo.
Hayo yameelezwa jana Desemba 13, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Godfred Mbanyi wakati akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Watahiniwa 610 sawa na asilimia 46.4 wamefaulu kati ya watahiniwa 1314 waliofanya mitihani ya kitaaluma, watahiniwa 663 sawa na asilimia 50.5 wanarudia masomo yao na watahiniwa 41 sawa na asilimia 3.1 wamefeli na wataanza upya masomo yao katika ngazi husika,” amesema.
Akizungumzia matokeo hayo, Mbayi amesema katika matokeo hayo, wanafunzi wawili walifutiwa matokeo baada ya kufanya udanganyifu katika kituo cha Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesisitiza kuwa adhabu kwa wanafunzi hao ni kutofanya mitihani katika vipindi vitatu mfululizo na endapo makosa hayo yatabainika tena, adhabu yake ni kufutiwa usajili na kutopata kazi zozote na ununuzi na ugavi.
“Nitoe wito kwa watahiniwa wetu wote kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani. Yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua na akibainika kurudia anaweza kufutiwa usajili na asifanye kazi zozote za ununuzi na ugavi.
Mbanyi amewaomba waajiri wote kutambua kuwa eneo la ununuzi na ugavi ni nyeti na Serikali imekuwa ikipata hoja nyingi na zingine zinashindwa kujibika kwa wakaguzi wanapokuwa eneo la ukaguzi kutokana na wengi wanaokaguliwa na wanaokagua kukosa weledi wa namna gani taratibu za ununuzi zinapaswa kuwa.