MABOSI wa Pamba Jiji hawatanii, kwani baada ya kumtambulisha wachezaji wapya watatu, Deus Kaseke, Habib Kyombo na Hamad Majimengi, sasa wanajiandaa kuwaweka hadharani nyota watano wa kigeni akiwamo kipa Mohammed Camara aliyekuwa Singida Black Stars na wengine walianza kutafutiwa vibali.
Mbali na Camara ambaye hakuwa anapata namba mbele ya Metacha Mnata wakati akiwa na Singida BS iliyomsajili mwanzoni mwa msimu huu, Pamba pia imewasajili mshambuliaji Mkenya, Mathew Teggisi Momanyi, Viungo Rally Bwalya kutoka Zambia na Mrundi Tshassiri Nahimana pamoja na beki Mcameroon, Cherif Ibrahim ambao wote hao wanaendelea kutafutiwa vibali vya kazi na vile vya kuishi ili kuwasha moto.
Pamba iliyopanda Ligi Kuu msimu huu baada ya msoto wa miaka 21 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imenasa kipa huyo raia wa Sierra Leone, aliyekuwa hana namba mbele ya Metacha Mnata na taarifa zinasema muda wowote Camara atatambulishwa na klabu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza.
Kipa huyo na nyota wengine wanne wa kigeni ni kati ya mastaa waliongezwa wakati dirisha dogo la usajili likifunguliwa rasmi leo, huku klabu hiyo ikihusishwa pia na beki mkongwe wa zamani wa Simba na Yanga, Kelvin Yondani atakayeunga ana kina Kaseke ambao tayari wameshaungana na kikosi hicho kujifua kwa jili ya mechi yao ijayo dhidi ya KMC itakayopigwa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo kwa sasa ipo nafasi ya 12 baada ya kucheza mechi 14, ikishinda mara mbili tu, huku ikipoteza sita sawa na sare ilizoambulia ikiwamo ile ya juzi dhidi ya JKT Tanzania.
Mabosi wa Pamba wamesema wameamua kuimarisha kikosi kwa nia ya kutaka kuona wanafanya vizuri katika duru lijalo la lala salama la ligi hiyo iliyopo raundi ya 14.
Mmoja wa viongozi wa Pamba aliyekataa kuandikwa jina gazeti alisema; “Hatujafanya vizuri mzunguko wa kwanza, ndiyo maana tunahitaji kupata wachezaji wengi wazoefu, watakaoongeza nguvu ya kuhakikisha timu inasalia Ligi Kuu.”
“Tayari wachezaji wapya waliotambulishwa wameshaanza mazoezi na timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mechi ijayo kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam,” aliongeza kigogo huyo wa klabu hiyo ambayo ni mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano.