Bunge la Korea Kusini limepiga kura Jumamosi kumuondoa madarakani Rais Yoon Suk Yeol, kutokana na jaribio lake lililoshindwa la kutangaza sheria ya kijeshi iliyodumu kwa muda mfupi.
Kati ya wabunge 300, wabunge 204 wamepiga kura ya kumuondoa rais madarakani kwa madai ya uasi, huku 85 wakipiga kura ya kupinga. Watatu hawakupiga kura, huku kura nane zikibatilishwa.
Spika wa Bunge Woo Won Shik, amesena kuondolewa kwa Yoon madarakani, ni matokeo yaliyochochewa na “hamu kubwa ya watu kuhusu demokrasia, ujasiri na kujitolea.”
Mamlaka na majukumu ya urais ya Yoon, sasa yamesitishwa na Waziri Mkuu Han Duck-soo atachukua uongozi wake pindi nakala za hati za kuondolewa kwake madarakani zitakapowasilishwa kwa Yoon na kwa Mahakama ya Katiba.
Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini ina hadi siku 180 kutoa uamuzi kuhusu mustakabali wa Yoon, ikiwa itamfukuza Rais, aua atarejeshewa mamlaka yake. Iwapo ataondolewa madarakani, uchaguzi wa taifa unapaswa kufanyika kumchagua mrithi wake ndani ya siku 60.
Hii ni mara ya pili kwa Bunge la Taifa kuipigia kura hoja ya kuondolewa Yoon. Jumamosi iliyopita, Yoon alisalimika kura ya kumuondoa madarakani, baada ya wabunge wengi wa chama tawala kuisusia kura hiyo.
Yoon asema kiti chake cha urais kimesitishwa ‘kwa muda’
Baada ya kura hiyo, Rais Yoon ametoa tarifa akisema “hatokata tamaa”, na amewataka maafisa kudumisha utulivu katika shughuli za kiserikali wakati wa kile alichokieleza kama “kusimama” kwa muda kwa urais wake.
”Napokea moyoni mwangu ukosoaji wote, kupewa pole na kutiwa moyo, na uungwaji mkono unaolekezwa kwangu. Nitafanya kila kilicho bora kwa ajili ya nchi yangu hadi dakika ya mwishi,” alibainisha Rais Yoon
Hata hiyo, akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni baada ya kura hiyo, Yoon amesema “ataachia ngazi”, lakini hakuomba radhi kutokana na jaribio lake hilo la kutangaza sheria ya kijeshi.
Kiongozi wa chama tawala cha Korea Kusini, Han Dong-hoon amesema anachukulia kwa uzito matokeo ya kura hiyo ya bunge kumuondoa madarakani Rais Yoon. Licha ya wito wa baadhi ya wabunge wa chama kujiuzulu kutokana na mgawanyiko ndani ya chama, Han amesema ataendelea na majukumu yake.
Waziri Mkuu wa Korea Kusini Han Duck-soo, ambaye sasa amekuwa kaimu rais, ameapa kuhakikisha utawala thabiti. Han ameahidi kwamba atafanya kila awezalo, kuiendesha serikali kwa utulivu, baada ya kura hiyo.
“Moyo wangu ni mzito sana. Ninajitolea kwa nguvu zangu zote na juhudi kuhakikisha kunakuwepo na utawala imara,” alisisitiza Han, wakati alipozungumza na waandishi habari Jumamosi baada ya kura hiyo ya bunge.
Spika wa Bunge Woo Won Shik, ameitaka serikali kushirikiana na kufanya kazi Pamoja ili kuleta utulivu wa uchumi na masuala ya kigeni.
Maelfu waandamana Seoul
Maelfu ya watu waliokusanyika karibu na majengo ya Bunge walishangilia kwa shangwe, huku wakipeperusha mabango. Wengine waliingia kwenye mitaa ya Seoul katika maandamano ya wanaomuunga mkono Yoon na wanaompinga, ambaye alitangaza jaribio lake hilo ambalo halikufanikiwa la kuweka sheria ya kijeshi Desemba 3.
Polisi inakadiria kuwa takribani watu 200,000 waliiingia kwenye mitaa ya Seoul kabla ya kura hiyo kupigwa.
Ama kwa upande mwingine, chama cha upinzani cha Korea Kusini cha Kidemokrasia, kimesherehekea na kupongeza hatua hiyo ya bunge ya kumuondoa madarakani Rais Yoon. “Kura ya le oni ushindi mkubwa wa watu,” alifafanua Park Cha-dae, kiongozi wa chama hicho.
(AFP, AP, DPA, Reuters)