Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema wizara yake kupitia vyombo vya usalama na taasisi nyingine za Serikali, zitashirikiana na vijana ili kupata suluhu kwa baadhi ya changamoto zilizopo na zinazoendelea kujitokeza katika jamii.
Changamoto hizo ni pamoja uhalifu, kupambana rushwa, dawa za kulevya, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Bashungwa aliyemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ameyasema hayo leo Desemba 14, 2024 wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa sita wa Chama cha Skauti Tanzania (TSA), uliofanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
“Tutaangalia hata kwenye taasisi ambazo viongozi wetu wa dini ni sehemu ya skauti Tanzania, tupanue wigo wa mtandao wa vijana katika makundi mbalimbali kwa kushirikiana na programu ya polisi jamii twende kwenye vijiji na kata tuhakikishe masuala ya kiuhalifu yanakomeshwa,”amesema.
Pia amesema watakaa na kuangalia makundi hayo kwa pamoja, jinsi ya kuyaratibu kwa namna wanavyoweza kuhakikisha wanasimamia maadili, kupinga ukatili wa kijinsia na utunzaji wa mazingira.
“Kwa haya yote tunaenda kuweka utaratibu maalum ambao tutakaa na kuangalia makundi ya vijana yaliyomo ndani ya Serikali, Skauti Tanzania na taasisi mbalimbali hata za dini ni namna gani tutashirikiana kuhahakikisha hatuliachii Jeshi la Polisi pekee katika ulinzi na usalama,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Skauti Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema, hivi karibuni licha ya chama hicho kufanya kazi vizuri, kilichafuka na hakutarajia machafuko makubwa kwa kiasi hicho.
Amesema alipoteuliwa kushika nafasi hiyo alikuta kuna kazi kubwa, lakini kilichomuumiza kichwa zaidi kilikuwa ni mgogoro wa skauti uliotokana na wanachama kutozingatia katiba na kanuni zao, jambo ambalo lilijenga ombwe lililosababisha mfarakano ndani ya chama hicho.
“Kwa kweli vita ya Skauti ni mbaya sana, kwa hiyo naomba tunapokwenda mbele tuhakikishe tunaheshimu katiba yetu na viongozi wetu. Tusithubutu kujenga taasisi ambayo ina ugomvi, mvutano na mfarakano ambao hauendani na hadhi ya mlezi wetu (Rais Samia Suluhu Hassan),” amesema.
Naye Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchata amesema katika mkutano wa Skauti Duniani uliofanyika katika mji wa Cairo, nchini Misri, Agosti mwaka, Tanzania ilitunukiwa tuzo ya ukuaji idadi ya wanachama na kuchukua nafasi ya kwanza katika bara la Afrika.
Amesema mkutano huo utapitisha rasimu ya mabadiliko ya katiba ya chama hicho ili kukidhi mahitaji ya sasa ya chama.
Pia mkutano huo utapitisha mabadiliko ya sera mbalimbali ikiwemo kuanzisha sera na tathimini ya usalama dhidi ya madhara ya unyanyasaji.