Simba kuna jambo, Fadlu achora ramani mpya

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kujiandaa kuikabili CS Sfaxien katika mechi ya tatu ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kesho Jumapili, lakini habari njema kwa Wanamsimbazi ni kitendo cha kocha Fadlu David kuchora ramani mpya ya mabao kabla ya kukabili watunisia hao.

Simba itakuwa wenyeji wa mechi hiyo ya Kundi A, ikiwa imevuna pointi tatu katika mechi mbili zilizopita, wakati wapinzani wao wakitoka patupu kwa kupoteza michezo miwili mfululizo na kila moja ina mabao mawili tu iliyofunga.

Wekundu hao walianza kwa ushindi wa 1-0 ikiwa Kwa Mkapa dhidi ya Bravos do Marqus ya Angola, kisha ikaenda kupokea kipigo cha 2-1 mjini Constantine, Algeria mbele ya CS Constantine, wakati Watunisia walianza kwa kulazwa 1-0 nyumbani na Constantine kisha kupigwa 3-2 ugenini na Bravos.

Katika kuhakikisha mambo yanakuwa freshi, Fadlu ameanza kupika mbinu mpya za kuwakabili Watunisia kupitia mazoezi wanayoyafanya kabla ya mchezo huo na kama Sfaxien haitajipanga si ajabu ikakumbana na kipigo kikubwa zaidi kuliko kile cha Angola.

Katika mazoezi ya juzi yaliyofanyika Kwa Mkapa utakaotumika kwa mchezo wa kesho, Fadlu aligeuka mbogo dhidi ya wachezaji wa kikosi hicho akiwataka wacheze soka la kasi, pia watengeneze na kutumia  nafasi ikiwa ni mbinu za kuwakimbiza Watunisia kesho mwanzo mwisho.

Ukiachana na kuwakimbiza muda wote, pia Fadlu alitaka kuona timu inafika haraka mwa adui fasta na alifoka pale walipopoteza nafasi akitaka kuwa makini zaidi.

Kule nyuma Fadlu, amekuwa akisimamisha mazoezi alipoona kosa limefanyika na kutaka kuwa, akiwaeleza wachezaji kuhakikisha safu ya kiungo cha chini wala mabeki hawatoi urahisi wa kuwapa nafasi Waarabu hao.

Akizungumzia hesabu za mchezo huo, Fadlu alisema kuna vitu viwili anavyovihitaji kesho dhidi ya Sfaxien nayo ni kumaliza mechi mapema kwa kufunga mabao ya haraka, pia kucheza soka la kasi kwa dakika zote 90.

Fadlu alisema, Sfaxien ni timu inayotumia mbinu za kuwalazimisha wenyeji kucheza kwa ‘tempo’ wanayoitaka, ili kuwapunguza kasi,, jambo ambalo hataki kuona kikosi chake kinaingia mtegoni.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini aliongeza, Sfaxien itatumia mashambulizi ya kushtukiza kutengeneza nafasi hatua ambayo itawalazimu kuwa imara na kucheza kwa nidhamu.

“Tunahitaji kufunga mabao, tulifanya makosa mechi iliyopita kule Algeria yaliyotuharibia hesabu zetu, tunatakiwa kufunga mabao ya kutosha japo najua haitakuwa mechi rahisi,” alisema Fadlu na kuongeza; “Hatutakiwi kukubali hilo lazima tucheze mpira wa haraka.”

Related Posts