Waajiri warudishwa darasani mfuko wa hifadhi ya jamii

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umewakumbusha waajiri kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Umesema wajibu huo ni pamoja na kutoa taarifa za wafanyakazi wasiosajiliwa kwa lengo la kutaka kuona Mfuko unakuwa na uwezo wa kuwasajili na kuwasilisha michango kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Desemba 14, 2024 na Meneja wa NSSF Mkoa wa Ubungo, Joseph Fungo wakati akifungua semina kwa waajiri wa sekta binafsi wanaohudumiwa na Ofisi ya NSSF Mkoa wa Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Fungo amewapongeza waajiri wa sekta binafsi kwa kushiriki semina hiyo yenye lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kwa waajiri pamoja na kuwakumbusha kutimiza wajibu wao.

Amesema suala la kutoa elimu kwa wanachama na waajiri wa sekta binafsi wa mkoa huo, litaimarisha ushirikiano kwa waajiri na Mfuko, sambamba na kuongeza mafanikio ya utoaji wa huduma bora kwa wanachama na wadau kwa ujumla.

Kwa upande wake, Ofisa Sheria wa NSSF, Geofrey Ngwembe amesema kuna umuhimu mkubwa kwa waajiri kuijua vema sheria ya hifadhi.

“Kuijua sheria hii ya hifadhi ni wajibu wa kila mwajiri ili aweze kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria hiyo,” amesema ofisa huyo.

Amesema mwajiri akiifahamu sambamba na kanuni zake za adhabu, atahakikisha michango ya wanachama inawasilishwa kwa wakati ili kukwepa adhabu zisizo za lazima.

Semina hiyo imefanyika kwa lengo la  kuwakumbusha waajiri majukumu yao yakiwamo ya kusajili  wafanyakazi wao na kuwasilisha michango kwa wakati kwa kuwa ni takwa la kisheria.

Katika semina hiyo, mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na matakwa ya Sheria ya Mfuko na matumizi ya mifumo ya Tehama iliyoboreshwa.

Related Posts