Shinyanga. Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imewataka viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji kuwachukulia hatua wananchi wanaotumia vyandarua kwa matumizi yasiyokusudiwa kama kufugia kuku, kuvulia samaki, au kuweka kwenye bustani za mboga. Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha leo Jumamosi Desemba 14, 2024, wakati wa mkutano wa waraghabishi kuhusu ugawaji wa vyandarua ngazi ya kaya.
Macha amesisitiza kuwa vyandarua vinatolewa kwa lengo la kudhibiti malaria, kutokana na Mkoa wa Shinyanga kuwa na maambukizi ya asilimia 16, ukiwa wa nne kitaifa kwa maambukizi hayo.
“Asilimia 70 ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga watanufaika na vyandarua bure vitakavyotolewa na Serikali, hatua inayolenga kupunguza maambukizi ya malaria,” amesema Macha.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Thimos Sosoma, zaidi ya vyandarua milioni 1.5 vimepokelewa kwa ajili ya kugawiwa bure kwa wananchi ili kuwakinga dhidi ya malaria.
Amesema utaratibu maalum wa kugawa vyandarua hivyo umewekwa kwa wananchi wanaoandikishwa ili kupata idadi sahihi ya walengwa katika kila eneo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Ofisa Miradi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Wilfred Mwafungu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, amesisitiza matumizi sahihi ya vyandarua na kueleza kuwa kampeni hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tamisemi.
Mratibu wa Malaria wa Mkoa, Beth Shayo amebainisha kuwa halmashauri zenye maambukizi makubwa ya malaria ni Ushetu, ikifuatiwa na Msalala, Shinyanga DC, Manispaa ya Kahama na Manispaa ya Shinyanga, huku Kishapu ikiwa na kiwango kidogo cha maambukizi.
Amesema sababu kuu za maambukizi hayo ni uwepo wa malambo mengi, misitu, visima vya wazi na shughuli za kiuchumi zinazochangia mazalia ya mbu.
Serikali imesisitiza matumizi sahihi ya vyandarua ili kufanikisha juhudi za kudhibiti malaria, ambayo bado ni changamoto kubwa kwa mkoa huo.