Mirerani. Serikali imewahakikishia wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini, kuwa haina mpango wa kuchukua madini yatakayobaki kwenye minada mbalimbali.
Aidha, imesisitiza kuwa dhana potofu kuhusu madini yaliyobaki baada ya mnada wa mwisho uliofanyika mwaka 2017 si ya kweli, kwani madini hayo yamehifadhiwa kwa salama katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na yatakabidhiwa kwa wamiliki halali.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Desemba 14, 2024 na Waziri wa Madini, Antony Mavunde wakati wa uzinduzi wa mnada wa ndani wa madini ya vito uliofanyika Mji Mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara.
Mnada wa madini ya vito ulikuwa umesimamishwa tangu mwaka 2017 kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza thamani ya madini hayo.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Serikali haitachukua madini yoyote yatakayobaki baada ya mnada, akieleza:
“Niko hapa kuwathibitishia hakuna madini ya mtu ambayo yatabaki baada ya mnada na kuchukuliwa na Serikali. Kumekuwa na dhana kwamba madini yaliyobaki mnada wa mwisho wa 2017 hayakurejeshwa kwa wahusika. Napenda kuwahakikishia kuwa madini yaliyokuwa Benki Kuu sasa tumeyatoa na tutawakabidhi rasmi wahusika ili waendelee na biashara zao.”
Waziri Mavunde ameongeza kuwa mnada huu ni msingi wa kujenga jukwaa la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla.
“Minada hii sasa itaendeshwa kwa njia ya kielektroniki ili kuhakikisha uwazi na ushindani. Serikali itaendelea kuimarisha masoko haya kwa kuendesha minada kwa uwazi,” amebainisha.
Amesema sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi na mchango wake katika mfuko mkuu wa Serikali uliongezeka kutoka Sh161 bilioni mwaka wa fedha 2015/16 hadi Sh753 bilioni mwaka wa fedha 2023/24.
Lengo ni kufikia Sh1 trilioni ifikapo mwaka wa fedha 2024/25.
Kuhusu madini ya Tanzanite, Waziri Mavunde amesema Serikali inachukua hatua za kurudisha hadhi ya madini hayo ili kushindana kimataifa, hatua ya kwanza ikiwa ni kurejesha minada ya ndani na kimataifa.
Aidha, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga kushughulikia malalamiko ya ucheleweshaji na changamoto za ukaguzi wa watu wanaoingia na kutoka katika eneo lenye ukuta wa Mirerani.
Thamani ya madini katika mnada
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema madini ya vito yenye uzito wa gramu 184.06 na thamani ya zaidi ya Sh3.1 bilioni, yanatarajiwa kuuzwa katika mnada huo.
Amesema mnada huo umevutia wauzaji 195, wakiwemo wachimbaji, wauzaji wa aina mbalimbali na waongezaji thamani.
Awali, Sendiga, alibainisha kuwa mnada huo utaongeza thamani ya madini na kuchangia uchumi wa eneo hilo, huku akieleza kuwa ujenzi wa soko la madini unaoendelea utaongeza tija kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Naye Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema bado kuna changamoto za ukaguzi katika ukuta wa Mirerani na ubovu wa miundombinu, akitaka hatua zichukuliwe kuboresha huduma hizo.