50 kuchuana Chadema kanda za Kaskazini, Kati

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imepitisha majina 50 ya wagombea watakaoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa kanda za Kaskazini na Kati.

Waliojitosa kugombea nafasi zikiwamo za uenyekiti, makamu mwenyekiti na mtunza hazina ni 22 kutoka Kanda ya Kaskazini na 28 wa Kanda ya Kati.

Uteuzi wa majina hayo ni kumalizia mchakato wa uchaguzi wa ngazi ya kanda hizo mbili zilizobakia baada ya nyingine nane kufanya uchaguzi na kupata safu mpya za uongozi.

Kikao cha Kamati Kuu kupitisha majina hayo kiliketi jana Desemba 14, 2024 kikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 15, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ibara ya 7.7.16(s).

“Kamati Kuu ya chama katika kikao chake cha Desemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam ilifanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa kanda za Kaskazini na Kati na kuteua wagombea wa uenyekiti, makamu mwenyekiti na mtunza hazina wa kanda,” imeeleza taarifa hiyo.

Wanaowania nafasi ya uenyekiti Kanda ya Kaskazini ni Anthony Mallya, Michael Kilawila na Samwel Welwel.

Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti wapo Gervas Sulle, Elifuraha Matela na Emanuel Landey, huku nafasi ya mhazini wapo Bahati Mollel na Emma Kimambo.

Kanda ya Kati majina nafasi ya uenyekiti ni ya David Djumbe, Devotha Minja, Ezekiel Chisinjila, Iddi Kizota na Shujaa Evarist.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ni Daniel Marwa, Godfrey Charles, Imelda Malley na Jingu Jackson, huku nafasi ya mhazini wapo Honest Masaki, Kapalatu Singamagazi na Modestus Chitemi.

Related Posts