Kwa pekee, leo tutadadavua ulazima, umuhimu na shuruti ya uaminifu katika ndoa. Japo ndoa huanza na mapenzi baina ya wawili, kinachofuatia ni uaminifu. Bila uaminifu ndoa si ndoa, bali doa.
Ndiyo maana kuna usemi kuwa ndoa ni ndoana. Hii inatokana na ukweli kuwa mhusika hujikuta amejifunga kwa mtu asiyefaa, hasa unapokosekana uaminifu. Katika ndoa lazima wahusika waaminiane kwanza.
Hebu fikiria. Unatoa maisha yako kwa mtu hadi kifo bila ushahidi kuwa itakuwa hivyo. Yote hii inatokana na uaminifu ulioujenga kwake. Je, naye huwa ni hivyo kwako? Swali hili lina majibu mengi, tena magumu kulingana na anayelijibu. Hivyo, hatutatoa jibu. Jibu toa mwenyewe.
Tumesema upendo ni msingi wa kwanza wa ndoa. Msingi wa pili ni uaminifu, hasa ikizingatiwa kuwa ndoa ina majaribu na mitahani mingi, iwe ya kijamii hata kiuchumi. Hivyo, wanaofunga ndoa, wahakikishe wanaaminiana na si kuaminiana tu, bali wahakikishe wanaaminika.
Kwa nini uaminifu ni lazima na muhimu katika ndoa? Chukulia mfano inatokea hali ya kuyumba kiuchumi, ugonjwa, kesi na mengine kama hayo. Kama wahusika hawaaminiani juu ya kupendana, hakuna atakayejitoa au kumvumilia mwenzake. Vitaibuka vishawishi ambavyo si rahisi kuvishinda kama hakuna uaminifu tena wa kweli.
Hakuna mtihani mkubwa kama kuyumba kiafya au kiuchumi. Hebu fikiria mwenzako wakati mnaoana alikuwa nazo. Mara ghafla, unatokea mkwamo kiuchumi. Kwanza, waliowazunguka wataanza kujua, kuhoji, kusengenya, hata kuwacheka wasijue haya ni mapito na mitihani vinavyolenga kuwaimarisha au kuwabomoa kama uaminifu utatoweka au kupungua. Ni wachache wanaofikiria sawasawa kulingana na maisha yanavyobadilika.
Hivyo, wapo watakaotaka kujua kunani hata kama hayawahusu. Hapa ndipo msingi mwingine wa usiri au kutunza siri za ndoa unapoingia na kufanya kazi au kukosekana na kuharibu kila kitu. Wahenga wanatuasa kuwa siri ya mtungi aijuaye kata.
Na hapa tusisitize. Ni kata pekee apaswaye kuijua na kuitunza siri ya mtungi. Siri ya mtungi usimwambie jiwe, kwani ataubomoa mtungi ukose.
Katika mkwamo, siri za ndoa zinapofuja, wapishi watakuwa wengi na kuharibu mchuzi. Kimsingi, unapokosekana uaminifu ambao hutokana na kwenda sambamba na kutojiamini wala kuchukua tahadhari dhidi ya hatari dhidi ya ndoa, ndoa itayumba hata kusambaratika.
Kama zilivyo taasisi zozote, lazima ziwe na kanuni, miiko, ithibati, uhuru, upekee, uaminifu, usiri na wivu. Ndoa ikikosa au kupungua vitu hivi hugeuka tegemezi na hatarishi. Ndoa inayoendeshwa kwa kutegemea ushauri na matakwa ya wasiohusika si imara wala salama.
Japo hatukani kuwepo kwa wana familia, jamii, marafiki, mashoga, na wengine, ndoa si mali yao wala haiendeshwi kwa mawazo wala matakwa yao. Kuwa na hao juu ni jambo la kawaida katika maisha ila, katika ndoa, si washirika.
Ndoa si ushirika na haina wala haihitaji ushirika. Ndoa inapoanza kuendeshwa kwa mawazo, misukumo, na ushauri wa marafiki, mashoga, hata ndugu, ujue iko hatarini.
Kuwakaribisha wahusika wasiohusika kuhusika katika ndoa yako ni dalili za kukosa uaminifu na kutojiamini. Mlikutana na kuapa wawili, siyo mia mbili.
Kila mtu ana mzigo wake. Ana haki na majukumu yake katika maisha yake ikiwemo ndoa. Na ndoa ni ya wanandoa. Ndio wajuao misingi, miiko, siri, thamani, na umuhimu wake. Ndoa si klabu.
Ina misingi, sababu na siri zake. Ndoa ni kama serikali. Ndiyo maana huiingii bila kuapishwa, kuonywa, na kupewa majukumu kadhalika yatakayokupata ukikiuka mambo au viapo hivi. Hapa mantiki ni rahisi na wazi.
Wanandoa ndio wanaojua sababu za kufunga ndoa. Ndio wajenzi hata wavunjaji wa ndoa. Kimsingi, adui wa kwanza wa ndoa ni wanandoa wenyewe, hasa pale wanapokiuka misingi yake.
Kwa waliofundwa wakafundika wanajua kuwa hata ukilala njaa, huna haja ya kuitangazia dunia hata kama wapo wazembe wanaokutangazia mambo yao. Kama mnavyolala wawili tu kwenye chumba chenu cha kulala, na ndoa pia, inapaswa iishie hukohuko.
Ndoa ni kama moyo kwa wawili. Kwani, hakuna ajuaye yaliyomo moyoni na lazima yaachwe huko. Tusisitize. Ndoa bila uaminifu na usiri si ndoa bali doa.