Bwana harusi anayedaiwa kupotea, Polisi yadai aliuza gari la jamaa yake kinyemela

Dar es Salaam. Ni utata, ndivyo unavyoweza kueleza kuhusu taarifa za kupotea bwana harusi, Peter Masawe ambaye Jeshi la Polisi linaeleza uchunguzi wa awali umebaini alikuwa na madeni na ameuza mali za watu.

Mbali ya taarifa ya Polisi, baadhi ya marafiki wa Masawe  anayejulikana zaidi kwa jina  la Vincent,  wanaeleza wakionyesha wasiwasi kutokana na mzunguko waliotumia walipomtafuta tangu alipopotea.

Victor Mawalla, akizungumza na Mwananchi leo Desemba 15, 2024 amesema alipigiwa simu na Vincent ambaye ni rafiki yake akamweleza  alikuwa Mbezi na kuna magari mawili yanamfuatilia, moja alilitaja ni Toyota Land Cruiser (Hardtop).

Amesema alimpatia ushauri aingie kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa taarifa.

“Nilivyomwambia hivyo alikubali akinitajia namba za gari lililokuwa likimfuatilia lakini baada ya kufuatilia ikabainika gari alilolitaja limepaki eneo la Ilala,” amesema Mawalla.

Amesema baada ya kufuatilia Jeshi la Polisi lilikamata gari na mmiliki ambaye alifika Dar es Salaam akitokea Kahama mkoani Shinyanga kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya magari ambaye alikuwa hafahamu chochote kuhusu kinachoendelea.

Kwa upande wake, Polisi katika taarifa iliyotolewa leo Desemba 15, kupitia kwa msemaji wake, David Misime limetoa ufafanuzi kulingana na ushahidi uliokusanywa kupitia kwa watu mbalimbali na kupitia uchunguzi wa kisayansi waliofanya hadi sasa.

“Taarifa hiyo imethibitisha kupotea kwa Vincent Massawe na zilifikishwa Kituo cha Polisi Kigamboni Novemba 19, 2024 na mke wake na upelelezi ulianza mara moja na kuthibitisha kuwa ni kweli alikuwa na harusi Novemba 16, 2024.

“Baada ya harusi alitafuta gari la kuwarejesha ndugu zake na wageni wengine Moshi mkoani Kilimanjaro,” amesema.

Kwa mujibu wa Misime ushahidi mwingine waliopata katika kufuatilia suala hilo wakati wa maandalizi ya harusi yake aliazima gari kwa jamaa yake ili limsaidie likiwa na namba T 642 EGU aina ya Toyota Ractis.

“Baada ya harusi hakurejesha gari hilo kwa mwenyewe badala yake Novemba 18 mwaka huu inadaiwa alikuwa anafuatiliwa na gari ambayo alikuwa anaitilia mashaka, ndiyo siku hiyohiyo aliuza gari hiyo kwa kiasi cha Sh9 milioni akalipwa Sh8 milioni ikabaki Sh1 milioni,” amesema.

Kamanda Misime amesema taarifa waliyoipa inaonyesha siku hiyohiyo alimtumia mke wake kiasi cha fedha ili alipe madeni mengine yaliyotokana na harusi ikiwemo Toyota Coaster aliyokodi kuwarejesha wageni wake Moshi.

Kamanda Misime amesema gari aina ya Toyota Ractis limefuatiliwa na limekamatwa, akieleza ushahidi mwingine unaonyesha Masawe pia anadaiwa na watu wengine wawili mmoja Sh53 milioni na mwingine Sh16 milioni.

“Ukweli wa tukio hili utafahamika muda si mrefu kama amejipoteza au la kulingana na mtiririko wa ushahidi ulivyo na hili linategemea hasa tukipata ukweli kutoka kwa mke wake, kwani inadaiwa anao ufahamu mkubwa wa jambo hili,” amesema.

Rafiki mwingine wa Vincent ambaye hakutaka jina lake litajwe amedai baada ya gari kukamatwa muhusika alisema hajawahi kumfuatilia mtu na amefika Dar es Salaam akitokea Kahama kwa ajili ya kununua vifaa vya magari.

“Mmiliki wa gari alikamatiwa Ilala wakati huo Vincent alipiga simu akiwa Mbezi hadi sasa hatuelewi ufuatiliaji ulikuaje na hapa tunazidi kuchanganyikiwa, maana watu wanapiga simu kuuliza kama amepatikana,” amesema.

Amedai ana madeni na kabla ya kupotea aliuza gari la ndugu yake alilopewa kwa ajili ya maandalizi ya harusi pasipo muhusika kujua kinachoendelea.

Inadaiwa na rafiki huyo kwamba, Vincent alimtumia wakala wa fedha kufanikisha uuzaji wa gari hilo.

Amesema baada ya kutoweka ndugu, jamaa na marafiki walitoa taarifa Polisi, huku mkewe akiwapigia simu marafiki kutaka kujua alipo.

“Tumezunguka kila sehemu tukipigiwa simu kuna maiti imepatikana huku tunakwenda hakuna hospitali tumekosa kuingia tuna kazi ya kuangalia maiti tu,” amesema.

Related Posts