Chuo cha ZOE chatoa mafunzo ya uongozi kwa vijana

Kibaha. Ili kukuza maarifa na maadili kwa jamii itakayolitumikia Taifa kwa nyanja mbalimbali na kuzingatia maadili na utu wema, Chuo cha maandiko ya biblia (ZOE) kilichopo Kibaha mkoani Pwani kimeanza kutoa mafunzo ya uongozi kwa vijana.

Akizungumza leo Jumapili, Desemba 15, 2024 kwenye mahafari ya 15 ya chuo hicho, Askofu wa Kanisa la Assemblies of God Dayosisi ya Mashariki, Laurence Kametta amesema mafunzo hayo yanasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha kundi la vijana ambao ni tegemeo muhimu la Taifa.

“Elimu ni ufunguo wa utawala na kiongozi mzuri ni yule anayeweza kuitumikia jamii kiroho na kimwili. Ili kufanikisha hilo, anapaswa kupata maarifa yenye misingi mizuri pamoja na kuishi kwa hofu ya Mungu,” amesema Dk Kametta.

Askofu Kametta ameongeza uongozi umejikita katika ngazi mbalimbali kuanzia familia, taasisi na Serikali na kila eneo linahitaji watu wenye busara, utii, uzalendo na maadili mema.

“Leo wanachuo 130 wamehitimu baada ya masomo ya ngazi mbalimbali, ikiwemo uongozi, maadili na masomo ya biblia. Jitihada hizi zinajikita zaidi kwa kundi la vijana,” ameeleza.

Baadhi ya wahitimu wamesema elimu waliyoipata imewaongezea maarifa na uwezo wa kutambua mema na mabaya kwa kutumia busara, jambo litakalokuwa na tija kwao binafsi na jamii inayowazunguka.

“Tofauti ipo kubwa nilivyokuja na sasa. Nimepata maarifa na mbinu zitakazonisaidia kuunganisha jamii yangu na kudumisha amani,” amesema Joyce Mwanika.

Kwa upande wake, Asnart Mtega ameitaka Serikali kuimarisha mikakati ya kudhibiti makanisa yanayoendesha huduma zao kinyume na maadili ya nchi ili kuhakikisha amani inadumishwa.

“Chanzo kikuu cha makanisa mengi kwenda kinyume na maadili ni viongozi wao kutokuwa na elimu ya masuala ya dini na uongozi, hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua za kuyadhibiti ili kuepuka migogoro katika jamii,” amesema Asnart.

Related Posts