KITENDO cha washambuliaji wa Songea United, Cyprian Kipenye na Ramadhan Kipalamoto kupitia changamoto ya kutokufunga kwa takribani michezo minne ya kikosi hicho, imemuibua kocha mkuu wa timu hiyo, Ivo Mapunda anayeeleza ni jambo la kawaida.
Mapunda aliyetamba na Yanga, Simba na Azam FC sambamba na kukipiga Taifa Stars na kucheza soka la kulipwa Ethiopia na Kenya, ameyasema hayo baada ya mabao manane kati ya 14 ya kikosi hicho msimu huu kufungwa na nyota hao, kila mmoja akitupia manne, japo kasi yao kwa siku za karibuni imepungua.
“Ni kweli kasi yao imepungua ila ni upepo mbaya tu ambao wanaokumbana nao na unaweza kumtokea kila mmoja wetu, unajua wao ni wachezaji wazuri hivyo, mabeki wa timu pinzani wamekuwa wakihakikisha wanawalinda ili wasiletewe madhara zaidi,” alisema Ivo.
Kocha huyo aliongeza jambo nzuri ni kuona wengine pia wakifunga akiwemo, Andrew Chamungu ambaye hakuanza msimu vizuri na kikosi hicho, ingawa hadi sasa tayari ameanza kuonyesha ubora wake, akifunga mabao manne sawa na Kipenye na Kipalamoto.
Timu hiyo ambayo zamani ilifahamika kwa jina la FGA Talents kisha kubadilishwa na kuhamishia makazi yake mkoani Ruvuma, kabla ya mechi ya jana dhidi ya Geita Gold, tayari imecheza michezo 11, ikishinda mitano, sare minne na kupoteza miwili.