UKISIKI Jumapili maalumu, basi ndiyo leo. Ndio leo ni Sunday Spesho kweli kweli kutokana na mechi za maana zitakazopigwa kuanzia hapa nyumbani Tanzania hadi barani Afrika na kule Ulaya. Yaani kama wewe ni shabiki wa soka, basi leo unapaswa ujishilie kuanzia saa 10 jioni hadi usiku mwingine.
Kama hujui, kuanzia muda huo, kutakuwa na vipute vya maana. Iwe unafuatilia mechi hizo ukiwa vibanda umiza au sebuleni kwake, hupaswi kumruhusu mtoto achezee rimoti kutokana na uhondo huo wa kufungia Jumapili.
Kama umesahau ni kule England kuna Dabi ya Manchester, wakati Man City itakuwa wenyeji wa Man United, huku kila moja ikiwa na mwenendo wake katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Lakini kabla ya wababe hao wa EPL hawajavaana hapo saa 1:30 jioni, mapema saa 10:00 jioni Kwa Mkapa kutakuwa na shughuli pevu wakati Mnyama Simba atashuka uwanjani kuvaana na CS Sfaxien ya Tunisia, ikiwa ni moja ya mechi nane za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Pia kumbuka kuna mechi nyingine mbili za kibabe za Ligi ya Mabingwa ikiwamo ya Mamelodi Sundowns ya Sauzi na Raja Casablanca ya Morocco.
Mechi ya Simba na Sfaxien ni ya aina yake kwani kila moja itakuwa ikihitaji kuvuna pointi tatu, baada ya zote kupoteza mechi zao zilizopita, Wekundu wakifumuliwa 2-1 ikiwa Algeria mbele ya CS Constantine, huku Watunisia hao walipoteza pambano la pili mfululizo kwa kulala 3-2 mbele ya Bravo do Maquis ya Angola, iliyoipa Simba pointi tatu katika mechi ya kwanza iliyopigwa Kwa Mkapa wiki mbili zilizopita.
Simba inayoshika nafasi ya pili katika Kundi A ikiwa na pointi tatu sawa na ilizonazo Bravos, inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kujiweka pazuri kuvuka kwenda robo fainali kwa mara nyingine baa ya kufanya hivyo mara tano katika misimu sita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Huu ni mchezo wa kwanza baina ya timu hizo, lakini kila moja ikiwa na rekodi za kusisimua katika michuano ya CAF, wageni wakiwa ndio vinara wa kubeba mara nyingi taji la Shirikisho ikifanya hivyo mara tatu, 2007, 2008 na 2013, huku 2010 ikifika fainali na kupoteza, mbali na kucheza nusu fainali za Ligi ya Mabingwa mara mbili tofauti huku ikitwaa Kombe la CAF 1998, ambalo Simba ilicheza fainali zake mwaka 1993.
Ukiacha kufika fainali ya Kombe la CAF, Simba pia imewahi kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa (enzi za Klabu Bingwa Afrika) mwaka 1974 na katika misimu sita iliyopita ya michuano ya CAF, imefika robo fainali mara tano ikiwamo msimu uliopita ilipocheza Ligi ya Mabingwa na kutolewa na Al Ahly waliotetea taji hilo.
Licha ya rekodi tamu ilizonazo Sfaxien, lakini katika makundi ya msimu huu imekuwa urojo ikiburuza mkia Kundi A, jambo linaloweza kuipa faida Simba inayojua kuutumia vyema uwanja wa nyumba wa Mkapa.
Simba ina wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanajivunia rekodi nzuri ya nyumbani, jambo linalowafanya kuwa na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki na kama itacheza kama ilivyocheza mchezo uliopita dhidi ya Constantine ni wazi pointi tatu zitawahusu kwani Watunisia wana ngome dhaifu inayoruhusu mabao.
Katika mechi tano zilizopita, Sfaxien imeshinda mechi mbili tu zote zikiwa za Ligi Kuu ya Tunisia, lakini ikipoteza mbili zote zikiwa za Kimbe la Shirikisho na imetoka sare moja ikiwa ni ya ligi ya kwao, wakati Simba katika idadi kama hiyo ya mechi tano, imeshinda nne bila kuruhusu bao na kupoteza moja ya CAF ilipolala 2-1 kwa Waalgeria mjini Constantine.
Akizungumzia mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar, kocha wa Simba, Fadlu David, alisema hakuna namna yoyote kwa kikosi chake ila kupata ushindi na ikiwezekana kwa idadi kubwa ya mabao.
“Tunahitaji pointi tatu, hii ni mechi muhimu na ngumu tunayotakiwa kushinda, tumekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa, kama nilivyosema mwanzo tutakuwa na mabadiliko ya kimbinu tofauti na mchezo uliopita. Nawaomba Wanasimba wajitokeze kwa wingi kutusapoti, kwa pamoja tunaweza. Simba nguvu moja.”
Kocha Fadlu aliyekuwa akifundisha soka huko Morocco na hivyo kuwa na uzoefu na aina ya soka linalochezwa na klabu za ukanda wa Afrika ya Kaskazini ataendelea kuwategemea nyota wa kikosi cha kwanza akiwamo, kipa Moussa Camara aliyefungwa mabao mawili tu hadi sasa katika michuano ya CAF.
Pia ana majembe kama Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua, Fabrice Ngoma na mabeki Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Fondoh Che Malone na Chamou Karaboue, bikla kusahau mawinga, Edwin Balua, Kibu Denis katika kuifungua ngome ya Sfaxien itakayosaka ushindi wa kwanza wa hatua ya makundi ikiwa ugenini.
Fadlu anajivunia mabeki wenye uwezo wa kuzuia na kuanzisha mashambulizi, huku eneo la kiungo likiwa na utulivu tofauti na eneo la ushambuliaji ambalo limekuwa lilikosa utulivu na umakini kiasi cha kuinyima Simba mabao katika mechi mbili zilizopita za kundi hilo, kwani bao iliyoifunga Bravos lilitokana na penalti ikifungwana Ahoua, huku bao la kufutia machozi Algeria lilifungwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Fadlu ameonyesha kupendelea mfumo wa 4-2-3-1, ambao ni mfumo wa kisasa wa soka unaotumika sana.
Mfumo huu unawaruhusu viungo wa kati wa Simba kuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo na kuwa na ufanisi mkubwa katika kushambulia na kulinda.
Katika mfumo huu, viungo wawili wa ulinzi, kama vile Ngoma na Okejepha, wanahakikisha kuwa Simba inaendelea kuwa imara kwenye eneo la kati, huku wakiwazuia wachezaji wa CS Sfaxien kufanya mashambulizi.
Kwa mbele, viungo wa kushambulia kama Kibu Denis, Ladaki Chasambi na Ahoua wanapata nafasi nzuri ya kushambulia na kutengeneza nafasi za mabao. Mfumo wa 4-2-3-1 pia unawawezesha wachezaji wa pembeni kuingia kwenye maeneo ya hatari kwa haraka na kuleta madhara kwenye lango la wapinzani.
Ikiwa Fadlu atatumia mfumo huu vizuri, utaweza kuwa na mafanikio makubwa kwa Simba, hasa ikizingatiwa kuwa wachezaji wa Simba wamezoea mfumo huu na wanaufahamu vyema.
Uwanja wa Benjamin Mkapa unatoa faida kubwa kwa Simba, hasa kutokana na uwepo wa mashabiki wao, pia ikibebwa zaidi na rekodi inpocheza Kwa Mkapa katika mechi za kimataifa.
Rekodi zinaonyesha tangu 2018 hadi msimu huu, Simba imecheza jumla ya mechi 35 za CAF na kupoteza mara tatu tu ilipolala 3-1 kwa Jwaneng Galaxy ya Botswana, ilazwa 3-0 na Raja Casabalanca kisha msimu uliopita ikafungwa na watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri, lakini ikishinda michezo 25.
Michezo hiyo 25 ni pamoja na miwili ya msimu huu, ikiilaza Al Ahli Tripoli ya Libya katika raundi ya pili kwa mabao 3-1 na wiki mbili zilizopita ikaicharaza Bravos kwa bao 1-0, ilihali michezo saba iliisha kwa sare ikiwamo ile ya michuano mipya ya Kombe la Afrika (AFL) na kufunga jumla ya mabao 73 na kufungwa 19.
Hii ina maana kama Simba itaendelea na moto huo kwa mechi za nyumbani, basi ni wazi Watunisia leo watapigwa kwenye mshono katika kidonda walichonacho cha kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita.