JK ndani ya Rombo Marathon & Ndafu Festival

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza maelfu ya wanariadha wa mbio za  Rombo Marathon 2024, zinazoenda sambamba na tamasha ya vyakula asilia zitakazofanyika Desemba 23, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala alisema wilaya hiyo imejipanga kupokea watu zaidi ya 3000 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro wakiwamo wanariadha wapatao 1200 watakaoshiriki mbio hizo.

“Tunatarajia kupata wanariadha 1200, sambamba na wakimbiaji wengine wa kawaida zaidi ya 3000 na mgeni rasmi atakuwa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete,” alisema DC Mwangwala na kuongeza;

“Niwahakikishie wale wote mtakaokuja Rombo marathon na wale mnaokuja kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka, najua kutakuwa na sherehe mbalimbali, niwahakikishie kutakuwa na amani na utulivu na ulinzi umeimarishwa.”

DC Mwangwala alisema fedha zitakazopatikana katika mbio hizo zitapelekwa kwenye ujenzi wa vyoo vya shule za msingi na sekondari, huku kiasi kingine kitaelekezwa katika ujenzi wa Hospitali ya Huruma lengo likiwa ni hospitali hiyo kuwa ya Rufaa kwa wilaya hiyo. 

Pamoja na mambo mengine, alisema siku hiyo kutakuwa na nyama choma festival na vyakula vya asili vya Kichaga ikiwemo ngararumu, mtori, kitawa machalari na vyakula vingine vya asili.

Mratibu wa mbio hizo, Temmy Masae alisema kutakuwa na mbio za kilomita 21, kilomita 10 na wanariadha hao watakimbia msituni na kilomita tano ambazo ni kama mtoko wa kifamilia.

Masae alisema wanariadha watakimbia katika maeneo ya Rongai, Tarakea ikiwa ni hifadhi ya msitu wa TFS wenye madhari nzuri ya kuvutia ikiwemo wanyama, maporomoko ya maji, misitu minene ya kuvutia na kuwakaribisha wadau na wanariadha kujitokeza kwani mbio hizo zina zawadi nono kwa washindi wake.

Related Posts