KenGold, Namungo moto utawaka, maafande wakishikana mashati Dar

UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa kushuhudiwa viwanja viwili vikiwaka moto, jijini Mbeya kuna pambano la vibonde wa ligi hiyo, wakati jijini Dar es Salaam kuna vita ya maafande, huku upande ukitamba kuondoka na pointi tatu.

Jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mapema saa 8:00 mchana KenGold inayoburuza mkia kwa muda mrefu sasa itakuwa wenyeji wa vibonde wengine wa ligi hiyo, Namungo iliyopo juu ya wachimba Dhahabu hao wa Mbeya, kabla ya saa 10:15 jioni JKT TZ na Mashujaa watashikana mashati jijini Dar es Salaam.

KenGold iliyopanda daraja msimu kutoka Ligi ya Championship, imekusanya pointi sita tu hadi sasa katika mechi 13 ilizocheza ikiwa imeshinda mara moja tu, ikitoka sare tatu na kupoteza michezo tisa, inavaana na Namungo iliyopisha naye pointi nne tu, Namungo huku kila moja ikitaka ushindi kujinasua ilipo.

Namungo inayonolewa na kocha Juma Mgunda yenyewe katika mechi 13, imeshinda tatu, kupoteza pia tisa na kuambulia sare moja iliyopatikana katika mchezo uliopita ugenini dhidi ya Kagera Sugar.

Hiyo ni mechi ya aina yake, kwani KenGold inajitaji ushindi ili kuongeza tumaini la kujinasua kutoka mkiani kabla ya duru la kwanza halijamalizika, kwani ikishinda itafikisha pointi tisa, na kupunguza pengo baina yao na Namungo iliyopo juu yake ambao pia wanataka kushinda ili watoke katika eneo hilo la hatari.

Rekodi zinonyesha kuwa Ken Gold ni moja ya timu zilizoshindwa kutumia viwanja vya nyumbani kuvuna pointi, kwani katika mechi sita ilizocheza Sokoine imeshinda mara moja tu, huku mechi tatu ililazimishwa sare na kupoteza miwili, ilihali Namungo rekodi kwa mechi za ugenini nao ni wachovu uikivuna pointi nne tu.

Pointi hizo za ugenini kwa Namungo ilikuwa ni kushinda mchezo mmoja na kutoka sare pia moja na kupoteza michezo minne katika ya sita iliyocheza, kuonyesha mchezo wa leo yeyote anaweza kucheka ikitumia vyema dakika 90 za pambano hilo.

Kocha wa KenGold, Omary Kapilima alishasema mapema kila mchezo kwao kwa sasa ni kama fainali kwa nia a kutafuta pointi za kuwanusuru wasirudi walipotoka, huku akiendelea kuwategemea nyota wake Joshua Ibrahim, Herbert Lukindo na Daudi Mishamo katika kufumani nyavu.

Nyota hao wamefunga jumla ya mabao saba kati ya nane iliyovuna KenGold katika mechi hizo 13 zilizopita, japo timu hiyo imekuwa ikiangushwa na ukuta mwepesi ulioruhusu mabao 22  ikiwa timu ya pili kwa kuruhusu idadi kubwa ya mabao baada ya Fountain Gate iliyofungwa 23 kupitia pia mechi 13.

Kwa upande wa Namungo ni moja ya timu zilizofunga idadi ndogo ya mabao ikifunga sita tu kama ilivyo kwa Tanzania Prisons, lakini imeruhusu mabao 16, huku ikiwa haina mchezaji maalum wa kuifungia mabao kitu ambacho hata kocha Juma Mgunda alishakieleza katika mahojiano na Mwanaspoti hivi karibuni.

Ukiachana na mchezo huo, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:15 jioni, JKT TZ itaikaribisha Mashujaa, huku zikiwa zinafuata katika msimamo zikitofautishwa na pointi moja tu, wageni kutoka Kigoma wakiwa na 18, ilihali wenyeji wana 17 na leo zitakuwa zikipimana ubavu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, likiwa ni pambano la tatu baina yao tangu Mashujaa ipande daraja msimu uliopita.

Katika mechi mechi mbili za msimu uliopita kila timi ilishinda nyumbani kwa bao 1-0, hii ni kuonyesha mchezo wa leo hautakuwa wa kawaida kwa timu hizo ambazo ni za vikosi vya majeshi.

Makocha wa pande zopte mbili, Ahmad Ally wa JKT na Abdallah Mohammed ‘Baresi’ kila mmoja amekiri mechi hiyo ni ngumu lakini wanatarajia kuvuna alama tatu ili ziwasaidie mbele ya safari, huku zikiwa hazijapishana sana katika matokeo katika mechi zao walizocheza hadi sasa katika ligi hiyo.

Mashujaa inayowategemea Crispin Ngushi, david Ulomi na Ismail Mgunda, katika mechi 12 ilizocheza imeshinda minne kama JKT, lakini imepata sare sita, ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo maafande wenzao waliocheza mechi 13, huku kila moja ikiwa imepoteza michezo mitatu.

JKT itaendelea kutegemea maajabu ya nahodha wa zamani wa Azam Fc na Simba, John Bocco kufunga mabao, sambamba na Hassan Kapalata, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na Edward Songo ili kuvuna alama tatu ikiwa nyumbani, lakini ikitakiwa kuwa makini na wageni kwani hawachagui kiwanja cha kubeba pointi.

Related Posts