Kilimajaro. Ongezeko la joto, mabadiliko ya vipindi vya mvua, na upungufu wa raslimali za asili vinaathiri uwezo wa wanyama kufuata mifumo ya hali ya hewa.
Jambo hili limeathiri wanyama kutafuta chakula na hivyo kuhamia maeneo mapya, hali inayoongeza hatari ya kutoweka au kushambuliwa na magonjwa. Haya ni mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri mifumo ya ikolojia ya wanyama.
Sera ya Taifa ya Uhifadhi Wanyamapori ya 1998, iliyopitiwa mwaka 2007, inalenga kulinda bioanuwai kwa kuanzisha hifadhi zinazowakilisha makazi asilia ya spishi zote muhimu.
Hata hivyo, sera hii inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ukame, na ongezeko la watu, ambavyo vinasababisha matumizi makubwa ya raslimali za kibiolojia kupitia kilimo, ufugaji, na ujenzi wa makazi.
Athari zinaonekana wazi katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,245. Ukame wa eneo hilo unasababisha wanyama kusafiri umbali mrefu kutafuta maji, hali inayochangia vifo.
Mhifadhi wa hifadhi hiyo Jackson Lyimo amesema “wanyama waliopo katika hatari ya kutoweka ni Faru Weusi, Mbwa Mwitu, Chitta, Chorowa na Swala Twiga hao ni wanyama adimu ambao wanapatikana hapa.
Kitu kinachotokea ni kwamba kama kutakuwa na ongezeko kubwa la joto linasababisha mtawanyiko duni wa malisho ya wanyama adimu unakuta hawapati mahitaji yao hasa malisho lakini pia maji kwa wakati inapelekea wanadhoofu,”amesema
Kwa mujibu wa Lyimo, jitihada za kuhifadhi wanyama hao zinafanyika, ikiwemo kuchimba mabwawa, kutumia magari ya kubeba maji (‘water boza’), na kutoa vyakula vya ziada kwa wanyama kama Faru Weusi.
Faru hao wamewekwa kwenye uzio maalum, na wanapokosa malisho ya asili kutokana na ukame, hupewa chakula mbadala ili kukidhi mahitaji yao ya lishe. Hizi ni juhudi za kuhakikisha spishi hizo adimu hazitoweki licha ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akifafanua wanyama wengine alisema “Lakini hawa Mbwa Mwitu ambao wapo kwenye uzio nao vilevile tunawalisha kwa sababu ili waendelee kuishi na kuzaliana tunahakikisha wanakula na kunywa”.
Mbwa Mwitu wapatikanao hifadhini hapo kawaida hupatiwa chakula kila siku ifikapo saa 11 jioni, huku kila mmoja akila kilo tatu za nyama.
Jitihada nyingine alisema, “Serikali inachukua hatua kuhakikisha wanapanda miti kwenye mazingira yanayozunguka hifadhi kwenye jamii ambazo awali walikuwa wanakata miti, huwa inakampeni maalumu ya kuotesha miti kila kaya waoteshe miti 20 na kuendelea”.
Licha ya jitihada hizo kufanyika Jackson anasema bado kuna changamoto kutoka kwa watu wasio na nia njema na uoto wa asili wanaoingia hifadhini kukata miti kwa matumizi ya nyumbani.
“Nashauri utoaji wa elimu uendelee kufanyika na kampeni za uoteshaji miti ziendelee pia serikali za vijiji zije na mpango maalumu za kutenge maeneo ya nyanda za malisho kwa ajili ya mifugo yao wasitegemee hifadhi” alisema.
Mhifadhi kitengo cha tiba ya Wanyama Mkomazi Violeth Kessy amesema mabadiliko ya tabianchi kwa wananyama husababisha ugonjwa wa kimeta ambao hutokana na ukame huku akitolea mfano ugonjwa huo pia ulisumbua hifadhi ya Tarangire.
“Mkomazi kuna uhaba wa maji, mfano kwa sasa kuna mabwawa machache sana ambayo tunayategemea na mengine yanaenda kukauka na mengine yalishakauka tulikuwa tunategemea mvua mwanzoni mwa mwezi wa tisa na kumi mpaka sasa zimechelewa ukame unatusumbua wanyama wanaathirika kwa kiwango kikubwa sana hatuna maji, nyasi zimekauka kwa hiyo wanyama wetu wanakufa.
“Hatujapata kiwango ‘incidence’ kikubwa sasa cha wanyama wetu kufa lakini kama hali itaendelea hivi badaaye itatusumbua kuna wanyama ambao hawawezi kustahimili hii hali wanakufa wengine wanakuwa wametoka umbali mrefu mpaka wanapokuja kuyafikia maji kutokana na kiangazi akinywa tu anaanguka anakufa,”amesema Violeth
Aidha katika hifadhi ya Mkomazi Violeth anasema wanategemea bwawa liitwalo Dindira.
“Tunalitegemea kwa mwaka mzima ndiyo linaweza kutunza maji lakini ilifikia mahali likawa linaenda kukauka ilibidi tuchimbe pembeni tutengeneze kingine kadogo kwa hiyo boza zinatoka zinaenda kupeleka maji,”amesema.
Akizungumzia jitihada zilizowekwa na serikali aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk Ashatu Kijaji katika ufunguzi wa Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) uliofanyika Septemba 2, 2024 mkoani Arusha alisema Tanzania imefanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na athari hizi kwa kupitisha sera na mipango mikakati ya kina.
Dk Kijaji alisema moja ya jitihada ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Kitaifa ya Mazingira (2021), Mpango Mkuu wa Kitaifa wa Masuala ya Kimkakati (2022-2032) pamoja na Sera ya Kitaifa ya Uchumi wa Buluu (2024).
“Ukweli ni kwamba mabadiliko ya tabianchi huleta athari kubwa, zinazojidhihirisha kupitia matukio mabaya ya hali ya hewa kama vile mafuriko, dhoruba, mvua zisizo na uhakika pamoja na uharibifu wa miundombinu,”alisema Dk Kijaji.
Mwanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi Chamtigiti Wakara amesema shughuli za kibinadamu zinachangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanaathiri mifumo ya kiikolojia, hifadhi za taifa, na mapori ya akiba.
“Kupitia upungufu wa mvua viumbe hai mwituni vinategemea kwa ajili ya kupata majo, makazi na chakula mvua zinapokuwa chache, chakula kikiwa kidogo hata uzalishaji wa wanyama unakuwa mdogo” alifafanua.
Pia, matumbawe baharini yanashindwa kuhimili ongezeko la joto, na ndege wa Flamingo katika Ziwa Natron wanakabiliwa na changamoto za upungufu wa chumvi inayohitajika kwa chakula chao, hali inayosababisha kupungua kwa idadi yao.
Chamtigiti ameongeza kuwa tafiti za mabadiliko ya tabianchi hukabiliwa na changamoto za rasilimali fedha, hivyo kuathiri utekelezaji wa utafiti wa kina unaohitaji vifaa vya kisasa na muda wa kutosha.
Akitilia mkazo suala hilo Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Wanyama Pori Mweka, Dk Emanuel Martin amesema elimu ya kutosha inatakiwa kutolewa kwa jamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
“Lazima watu wajifunze kutunza mazingira wapande miti ya kutosha ili kupunguza hewa ya ukaa vilevile shughuli ambazo zinaongeza cabon badala ya kila mtu kuendesha gari basi tupande usafiri wa umma ili kupunguza uchafuzi huo, waache kukata miti watumie majiko banifu ambayo yanatumia mkaa kidogo na kuni kidogo.
“Sambamba na hilo mataifa makubwa yahakikishe yanachukua juhudi za makusudi za kupunguza hewa ya ukaa pia watu wapunguze kutumia madawa ya kuulia wadudu,”amesema Dk Martin.
Naye Mchambuzi na mtaalamu wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Rose Senyagwa amesema mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa hali ya hewa na wananchi kwa ujumla kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa kuwa athari zake zimepelekea kuathiri mifumo ya hali ya hewa na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa mfano vipindi vya mvua kubwa na ukame.
“Juhudi ambazo zinaendelea kufanyika ni kuongeza uangazi wa hali ya hewa (kwa ajili ya kupata takwimu za kutambua uwepo na kiwango cha mabadiliko). Kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa tabianchi (climate scientists), utoaji wa taarifa za mapema (early warning systems). Hii inasaidia wananchi kujiandaa na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa.
“Kutoa taarifa ya tabianchi kwa mwaka (annual climate report), kuelimisha Uma juu ya uwepo na athari katika majukwaa mbalimbali ikiwemo Nanenane, vikao vya wadau, mahojiano kwenye redio au runinga, n.k.) pamoja na utafiti na uchambuzi wa mbadiliko ya tabianchi,”ameeleza Rose
Hakuacha kutoa rai kwa jamii kufuatilia, kusoma na kutafsiri taarifa na tabiri za hali ya hewa na tabianchi.
“Kufuata ushauri unaoambatana na taarifa hizi kutoka TMA na pia mamlaka husika. Kutumia njia mbadala katika shughuli za kiuchumi na kijamii (kilimo cha umwagiliaji, mazao yanayoendana na tabianchi au himilivu, n.k.),”ameeleza Rose
Kwa upande wake Mhifadhi Daraja la pili kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Omary Mollel amesema mamlaka hiyo inapambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya hifadhi.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi ya uhifadhi wa mazingira na kuchukua hatua mbalimbali kama kuchimba mabwawa katika maeneo ya Hifadhi.”amesema.
Huku akiitaka jamii kuacha au kupunguza visababishi vya madhara ya tabia nchi pamoja na kupanda miti.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.