TOFAUTI na matarajio ya viongozi na hata mashabiki na wapenzi wa Simba wakati anasajiliwa, ukweli ni kwamba Mzambia Joshua Mutale anahesabu siku tangu dirisha dogo la usajili likifunguliwa leo, kutokana na kinachoelezwa majeraha ya mara kwa mara yanaweza kumng’oa Msimbazi.
Mutale alisajiliwa kwa mbwembwe katika dirisha kubwa la msimu huu, lakini ameshindwa kufanya maajabu akiwa hana bao lolote katika Ligi Kuu, kitu kinachoelezwa kimewafanya mabosi wa klabu hiyo kufikiria kumpiga chini ili nafasi yake aletwe mtu wa maana wa kuisaidia timu hiyo inayosaka heshima baada ya misimu mitatu mfululizo kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Mutale alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Power Dynamos ya Zambia hana mwendelezo wa kucheza mara kwa mara kutokana na majeraha ya mara kwa mara.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti, huenda majeraha yakawabadilisha mawazo ya kuendelea kuwa na mchezaji huyo hasa kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
“Amekosa muendelezo mzuri wa kucheza mara kwa mara, licha ya kupata nafasi anaweza akacheza mechi mbili au moja akakaa nje ya uwanja siku nne hadi tano timu inahitaji wachezaji wanaowajibika,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe na kuongeza;
“Mipango ya usajili inaendelea kimya kimya uwezekano wa kupunguza na kuongeza wachezaji wengine ni mkubwa kwani kuna wachezaji hawajafanya kile tulikuwa tunakitarajia.’’
Chanzo hicho kiliongeza kuwa endapo Simba itahitaji kuongeza wachezaji wa kigeni dirisha hili italazimika kuachana na baadhi ya wachezaji ili waweze kupisha usajili mpya hivyo mipango ya kufanya hivyo ikiendelea na wao wanaumiza kichea ni wachezaji gani wataachana nao.
Simba tayari ina wachezaji 12 wa kigeni kama kanuni ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) inavyotaka na ikielezwa kipa Ayoub Lakred atatemwa ili kumuachia nafasi Ellie Mpanzu aliyesajiliwa saa chache baada ya dirisha kubwa la usajili kufungwa Januari 15.
Nyota wa kigeni waliopo sasa Simba ukimuondoa Lakred ni, Moussa Camara, Valentin Nouma, Chamou Karaboue, Fondoh Che Malone, Augustine Okejepha, Debora Fernandez, Fabrice Ngoma, Steven Mukwala Joshua Mutale, Charles Ahoua na Lionel Ateba.