NYOTA wa gofu kutoka klabu mbalimbali nchini wanaanza kuwasili Dar kuanzia leo kushiriki mashindano ya Lina PG Tour yanayokamilisha raundi ya tano, kwenye viwanja vya Dar Gymkhana.
Raundi hii itaamua nani anastahili kubeba ubingwa wa jumla kwa gofu ya ridhaa na ile ya kulipwa.
Akifafanua kuhusu mashindano hayo, Yasmin Challi, mkurugenzi wa Lina PG Tour, alisema; “Mashindano haya yanajulikana rasmi kama Pro Am maana yake yanajumuisha wachezaji wa kulipwa (Professionals) na wale wa ridhaa (Amateurs).
Kwa upande wa gofu ya kulipwa, raundi ya tano itakuwa ni mchuano mkali kati ya Nuru Mollel, Fadhil Nkya na Isack Wanyeche wakati kwa upande wa gofu ya ridhaa, mchuano mkali upo kai ya Ally Isanzu, na Isiaka Daudi Mtubwi.
Mollel ambaye tayari ameshinda raundi tatu katika ya tano za Lina PG Tour, yuko katika nafasi nzuri ya kumaliza mshindi wa jumla hata kama asiposhinda raundi ya mwisho ambayo itaanza kuchezwa katika viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana kuanzia Disemba 19 hadi 22 mwaka huu.
Road to Dubai ndiyo kauli ya mbiu Lina PG Tour ambaye mshindi wake wa jumla atakata tiketi ya kucheza mashindano yenye hadhi ya kidunia jijini Dubai, Falme za Kiarabu.