Tangu mwaka 2021, kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda limechukua maeneo makubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), likisababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuzusha mgogoro wa kibinadamu.
Kulikuwa na matarajio makubwa kwamba mkutano ulioandaliwa na Rais wa Angola, Joao Lourenço — mpatanishi wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya kumaliza mzozo huo — ungemalizika kwa makubaliano ya kumaliza mgogoro.
Hata hivyo, karibu saa sita mchana Jumapili, mkuu wa ofisi ya habari ya Rais wa Angola alisema mkutano huo hautaendelea. “Kinyume na matarajio yetu, mkutano hautafanyika leo,” alisema afisa habari Mario Jorge kwa waandishi wa habari.
Lourenço alikuwa akikutana na kiongozi wa DRC, Felix Tshisekedi, bila uwepo wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alisema.
Ofisi ya rais wa DRC ilisema mazungumzo yamekwama kutokana na madai ya Rwanda kwamba DRC ifanye mazungumzo ya moja kwa moja na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Kigali, ambao tangu 2021 wamechukua maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC.
“Kuna mkwamo kwa sababu Wanyarwanda wameweka kama sharti la kusaini makubaliano kwamba DRC ifanye mazungumzo ya moja kwa moja na M23,” alisema msemaji wa Rais wa DRC, Giscard Kusema, aliyekuwa Luanda, katika mahojiano na AFP.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alisema Ijumaa kwamba nchi yake inataka “ahadi madhubuti kutoka DRC ya kurejea kwenye mazungumzo ya moja kwa moja na M23 kwa mfumo na muda uliowekwa wazi.” Hata hivyo, serikali ya DRC inasema kuwa M23 ipo tu kwa sababu ya msaada wa kijeshi kutoka Rwanda.
Somam pia: Waziri wa Kongo ataka kumkamata Kagame, akimwita “mhalifu”
“Ikiwa Kigali itakuwa na nia njema katika mazungumzo na itatimiza ahadi yake ya kuondoa wanajeshi wake kutoka ardhi ya Kongo, mgogoro na M23 utamalizika, na wakati huo huo utamalizika pia na Rwanda,” kilisema chanzo kutoka serikali ya DRC.
Kagame na Tshisekedi: Mvutano wa kisiasa na vita mashariki mwa DRC
Kagame na Tshisekedi walikutana mara ya mwisho Oktoba jijini Paris lakini hawakuzungumza moja kwa moja, huku mazungumzo yao yakiendelea kupitia upatanishi wa Luanda.
Mwezi Agosti, Angola ilisaidia kusimamia makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano ambayo yaliweka utulivu wa muda mfupi katika uwanja wa mapambano, lakini mapigano yameongezeka tangu mwishoni mwa Oktoba.
Eneo la Mashariki mwa DRC, lenye utajiri mkubwa wa madini, limekumbwa na vurugu za ndani na za mipakani kwa zaidi ya miongo mitatu, huku likiwa na makundi kadhaa ya waasi.
Jumatano, Tshisekedi alisema bungeni kuwa, “nchi yetu inaendelea kukabiliwa na uasi wa mara kwa mara, ikiwemo uvamizi wa jeshi la Rwanda na magaidi wa M23,” akiwaita wapiganaji hao na Rwanda “maadui wa Jamhuri.”
Soma pia: Waasi wa M23 wakaribia jimbo lenye utajiri wa madini Kongo
Mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ambao una takriban watu milioni moja na wengine milioni moja waliokimbia vita, sasa umekaribia kuzingirwa na waasi wa M23 na jeshi la Rwanda.
Mapema Novemba, majirani hao wawili walizindua kamati ya kufuatilia ukiukwaji wa usitishaji mapigano, ikiongozwa na Angola na kushirikisha wawakilishi wa DRC na Rwanda. Kinshasa na Kigali baadaye walikubaliana hati inayoelezea masharti ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda kutoka ardhi ya DRC.
Hata hivyo, hati ya awali ya Agosti iliyoeleza kuvunjwa kwa kundi la FDLR, lililoundwa na Wahutu waliokuwa sehemu ya mauaji ya kimbari ya 1994, kama sharti la kuondoka kwa Rwanda, ilikataliwa na DRC.
Hati ya mwisho, iliyoonekana na AFP, inapanga kipindi cha siku 90 “kukamilisha utokomezaji wa FDLR na kuondoa hatua za ulinzi za Rwanda.”
Chanzo: AFP