Namungo yaiduwaza KenGold | Mwanaspoti

LICHA ya kutangulia kwa mabao mawili ndani ya dakika 10 za pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, timu ya KenGold imejikuta ikiduwazwa na wageni na kupoteza mchezo huo ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa kwa kufungwa maao 3-2.

KenGold inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda msimu huu kutoka Ligi ya Championship, iliiduwaza Namungo kwa kufunga mabao mawili ya chapuchapu dk ya pili na ya tisa kupitia washambuliaji wao hatari, Mishamo Daudi na Joshua Ibrahim, kabla ya wageni kuzinduka na kupindua meza.

Mishamo alianza kuitanguliza KenGold kwa bao la dk ya pili, kabla ya Joshua kuongeza jingine akimaliza pasi ya Herbert Lukindo na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kuamini wangeweza kuibuka na ushindi mnono katika mechi hiyo, ila mambo yaliwabadilikia baada ya Namungo kurudisha mabao hayo kabla ya mapumziko.

Penalti ya dakika ya 26 iliyofungwa na mkongwe, Erasto Nyoni baada ya Jacob Massawe kuangushwa alipokuwa akienda kumsalimia kipa wa Kengold, Castor Mhagama na mwamuzi Nassor Mwinchui kuamuru pigo hilo na mpigaji huyo aliukwamisha kushoto mwa kipa huyo aliyeonekana kuufuata lakini kasi ya shuti ilimshinda kuuzuia usitinge nyavuni.

Wakati KenGold ikijiuliza kulikoni tena, dakika 10 baadae Fabrice Ngoy alitupia chuma cha pili akimaliza pasi tamu ya Pius Buswita na kuufanya mchezo huo kuwa mtamu zaidi, kwani hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni 2-2 kabla ya kipindi cha pili Namungo kutumia sekunde za mwisho kubeba pointi zote tatu.

Bao hilo la tatu liliwekwa tena kimiani na mkongwe Erasto Nyoni baada ya Buswita kuangushwa ndani ya boksi la KenGold na mwamuzi kuamuru pigo jingine na mkongwe huyo akamtesa kwa kupiga shuti la juu lilioenda kupita katikati ya lango hilo, huku kipa Castor akienda kushoto baada ya kudanganywa na mpigaji.

Matokeo hayo yameifanya KenGold kuendelea kubaki mkiani ikiwa na pointi sita baada ya mechi 14 sawa na ilizocheza Namungo ambayo imefikisha pointi 13 na kuchupa kutoka nafasi ya pili kutoka mkiani hadi ya 12.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho kwa michezo miwili, mapema saa 8:00 mchana Tanzania Prisons itakuwa wenyeji wa Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kabla ya KMC na Pamba Jiji kukwazana baadae saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar.

Keshokutwa Jumanne kutakuwa pia na mechi mbili wakati Tabora United itakapokuwa wenyeji wa Coastal Union kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kabla ya Azam kuikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Related Posts