Odinga alitoa kauli hiyo wakati wa mjadala wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mjadala huo uliwashirikisha wagombea wengine wawili, Mahamoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti na Richard Randriamandrato, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar.
Katika mjadala huo, wagombea walieleza maono na mikakati yao ya kubadilisha Afrika endapo watachaguliwa kushika nafasi hiyo Februari 2025, kumrithi Moussa Faki wa Chad.
Aidha, walijadili jinsi ya kutekeleza Ajenda ya Afrika ya 2063 inayolenga bara lenye ustawi, umoja, amani na linaloendeshwa na watu wake.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alibainisha kwamba Afrika inapaswa kuwa na uwakilishi wa kudumu ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na kura ya veto.
Odinga alisema: “Afrika, yenye wanachama 55 na idadi ya watu takriban bilioni 1.4, inapaswa kuwa na nafasi ya maamuzi katika chombo hicho muhimu cha kimataifa.
Alieleza kuwa Baraza la Usalama, lenye jumla ya wajumbe 15, linapaswa kuacha mfumo wa sasa ambapo wajumbe watano wa kudumu (China, Marekani, Ufaransa, Uingereza, na Urusi) pekee wana mamlaka ya kura ya veto.
“Hali ya sasa haizingatii mabadiliko ya ulimwengu tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa mwaka 1945 wakati nchi nyingi za Afrika zilikuwa makoloni,” alisema Odinga.
Odinga alisisitiza kuwa Afrika inahitaji viti viwili vya kudumu vyenye mamlaka ya kura ya veto ili kulinda masilahi ya bara hilo.
“Hatua ya Ulaya kuwa na viti vitatu vya kudumu huku Afrika ikikosa uwakilishi wa kudumu si haki. Umoja wa Mataifa lazima uakisi hali halisi ya dunia ya sasa,” alisema.
Asili ya neno “veto” ni Kilatini likimaanisha “ninakataza.” Katika Baraza la Usalama, kura ya veto hutumiwa kuzuia maazimio, hata kama yamekubaliwa na wajumbe wengi.
Kauli ya Odinga ilifanana na wito wa Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja, aliyetoa hoja kwenye mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Septemba, mwaka huu jijini New York.
Nabbanja alisema, “Afrika inastahili viti viwili vya kudumu vyenye kura ya veto na viwili vya mzunguko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”
Nabbanja alisisitiza kuwa mageuzi ya haraka na ya kina yanahitajika katika Baraza la Usalama, ili kuleta usawa wa uwakilishi.
Aliongeza kuwa ushindani na makabiliano kati ya mataifa makubwa yanadhoofisha juhudi za pamoja za kimataifa katika kuhakikisha usalama, amani na maendeleo.
Marekani, moja ya mataifa yenye kura ya veto, inaunga mkono pendekezo la Afrika kuwa na viti viwili vya kudumu, lakini bila mamlaka ya kura ya veto.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, alisema: “Marekani inatetea Afrika kupata viti viwili vya kudumu, lakini visivyo na kura ya veto, pamoja na kiti kimoja cha mzunguko kwa mataifa madogo ya visiwa vinavyoendelea.”
Alisema pia Marekani inaunga mkono India, Japan, na Ujerumani kupata viti vya kudumu.
Hata hivyo, Thomas-Greenfield alibainisha kuwa Washington haiungi mkono kuongeza mamlaka ya kura ya veto kwa zaidi ya mataifa matano yaliyopo sasa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilianzishwa mwaka 1945 likiwa na wanachama 11. Idadi hiyo iliongezeka hadi 15 mwaka 1965.
Wanachama kumi huchaguliwa kwa mihula ya miaka miwili, huku watano wakiwa wanachama wa kudumu wenye kura ya veto.
Pendekezo la Afrika kuhusu viti vya kudumu linachukuliwa kuwa hatua muhimu kuelekea usawa wa uwakilishi katika mfumo wa kimataifa, huku likibaki suala nyeti kwa mabadiliko ya kimuundo ya Umoja wa Mataifa.
Pia, Odinga alieleza jinsi muundo wa kifedha wa kimataifa ulivyokuwa mzigo mkubwa kwa nchi za Kiafrika, ambazo mara nyingi zinalazimika kukopa mikopo kwa viwango vya juu vya riba.
Odinga alipendekeza njia mbadala za ufadhili ambazo zingeziwezesha nchi za Afrika kuanzisha hazina ya kikanda ya kukopa kwa viwango vya chini vya riba.
“Muundo wa kimataifa wa ufadhili umeathiri vibaya Afrika, ambapo nchi za bara hili zinakopa kwa viwango vya juu vya riba ikilinganishwa na mataifa mengine. Tunahitaji kuchukua hatua madhubuti kushughulikia changamoto hii.
“Afrika ni bara lenye utajiri wa rasilimali, lakini bado linakabiliwa na umasikini mkubwa kwa viwango vya maisha,” alisema Odinga.
Matamshi yake yalilingana na kauli ya Rais William Ruto wa Kenya, ambaye amekuwa akisisitiza umuhimu wa mageuzi ya muundo wa kifedha duniani ili kutatua changamoto za kiuchumi zinazoikumba Afrika.
Kwa miezi kadhaa, Rais Ruto amekuwa akikosoa mtazamo wa mataifa ya kigeni kwa kuitaja Afrika kama mkopaji hatari, licha ya utajiri mkubwa wa maliasili unaopatikana barani humo. Ruto ametaka bara la Afrika kupewa nafasi ya kutumia kikamilifu rasilimali zake kuleta maendeleo na kubadilisha uwezo wake kuwa fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake Randriamandrato alitoa wito kwa nchi wanachama kuungana na kutoa msimamo thabiti katika kuchagua wawakilishi wa Afrika kwa ajili ya Baraza la Usalama la Umoja la Mataifa.
Aliyataka mataifa kuchukua udhibiti wa usalama wao wa ndani, akionya kuwa kambi za kijeshi za kigeni zinapaswa kuchukuliwa kuwa zimepitwa na wakati, kwani zinaweza kusababisha migogoro zaidi.
Randriamandrato aliangazia jukumu muhimu la kambi za kiuchumi za kikanda, kama vile Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, katika kuwezesha biashara katika bara zima.
Kwa upande wake Youssouf, alisisitiza kwamba kuimarisha usalama wa kikanda kunaweza kupatikana kwa kuongeza rasilimali kwa kikosi cha kusubiri, na hivyo kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
“Nchi jirani zinapokosa lengo la umoja, amani iko hatarini,” alisema Youssouf.
Youssouf aliwasilisha pendekezo la mfumo wa fidia wa malipo ulioundwa ili kuzuia nchi kupata hasara wakati wa kufanya biashara katika sarafu tofauti, akihoji: “Kwa nini usizingatie sarafu moja?”
Alidokeza kuwa mageuzi muhimu ndani ya umoja huo kwa sasa yanazuiwa na changamoto za ufadhili, akisema: “Hali hii lazima ibadilike,” na kufafanua kuwa hataweka suluhu kwa nchi wanachama lakini badala yake “atatetea.”