Polisi Tanzania yapiga mkwara mzito

KICHAPO cha mabao 4-0 ilichopata Maafande wa Polisi Tanzania dhidi ya Mbeya City juzi, kimeonekana kumchanganya kocha wa timu hiyo, Bernard Fabian ambaye ameweka wazi michezo mitatu ijayo ya kumalizia mzunguko wa kwanza ni lazima kieleweke.

Kocha huyo alisema katika michezo mitatu, miwili kati ya hiyo ni ya nyumbani ambayo wanaenda kufanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wao na Mbeya City, ili kuhakikisha wanapata pointi sita zitakazofufua matumaini kwao.

“Bado ni mapema kukata tamaa kwa sababu Ligi haijaisha na lolote linaweza kutokea, kimsingi tunaenda kujipanga tena upya kusahihisha makosa yaliyotokea hususani eneo letu la ulinzi na kuongeza makali ya washambuliaji wetu,” alisema Fabian.

Fabian aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Tabora United akichukua nafasi ya John Tamba, alikiri licha ya ugumu uliopo, ila kama benchi la ufundi wamejipanga kutengeneza kikosi cha ushindani huku akiomba sapoti ya mashabiki zao.

Katika michezo mitatu inayofuata kwa Polisi itaikaribisha Songea United Desemba 22, kisha itaifuata Stand United Desemba 28 na kumalizia raundi ya kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa Ushirika kwa kucheza na Biashara United Januari 10, mwakani.

Related Posts